Mbunge
wa Moshi Mjini, Japhary Michael, ameeleza kusikitishwa kwake juu ya
maofisa usalama kuwazuia yeye na Meya wa Manispaa hiyo kuingia Ikulu
ndogo ya Moshi kuhudhuria kikao cha Rais John Magufuli na viongozi wa
dini.
Michael
ambaye ni wa Chadema, alisema tukio hilo lilitokea juzi baada ya kufika
Ikulu kutokana na mwaliko wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kushiriki
kikao hicho.
Mbunge
huyo alisema aliitika mwaliko huo lakini ghafla akiwa kwenye foleni
yeye na Meya wakazuiwa kuingia na kutakiwa warudi walikotoka.
Alisema alifika eneo la tukio saa 6.30 mchana akamkuta Mstahiki Meya akiwa ametangulia kwenye foleni.
“Tulipata
mwaliko na tukaheshimu, ila katika mazingira ambayo hayaeleweki
tulizuiwa na watu wa usalama na sisi hatukuhitaji kugoma tukaondoka,” alisema.
Alisema
jambo la kusikitisha wakati akiwa kwenye foleni na viongozi wa dini,
viongozi wa CCM na watendaji wengine wa Serikali, alichomolewa yeye na
Mstahiki Meya wakiambiwa hawastahili kushiriki kika hicho.
Alisema
Mkurugenzi alijaribu kuwatetea kwa kuwambia ndiye aliyewapa mwaliko kwa
maelekezo ya Katibu Tawala wa Mkoa, hakusikilizwa kabisa.
“Mimi
mbunge sijaumizwa, kwa kuwa nimetimuliwa bali ninasikitika kwa kuwa
tunatiwa woga wa kushiriki shughuli za viongozi wetu wa kitaifa hasa
wanapofanya ziara katika maeneo tunayowakilisha,” alisema.
Alisema
kutokana na tukio hilo, huenda jamii ikawajengea taswira mbaya kwamba
hawaheshimu viongozi wa kitaifa pale wasiposhiriki matukio mengine.
“Mimi binafsi nimetafsiri tukio hilo lililonipata kama ubaguzi wa kiitikadi kwa mambo ambayo ni ya kitaifa,” alisema.
No comments:
Post a Comment