Thursday, May 11, 2017

MACHINJIO 7 YAFUNGIWA NA TFDA


Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imefungia machinjio saba, yakiwamo sita ya nguruwe na ng’ombe kutokana na ukiukaji wa sheria, ikiwamo uchafuzi wa mazingira na ukosefu wa majengo.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkaguzi wa TFDA, Dk. Itikija Mwanga, alisema mamlaka hiyo iko katika ukaguzi wa kawaida wa wiki mbili na kwamba wamebaini changamoto mbalimbali katika machinjio ya jijini.
Alisema tatizo kubwa ambalo wanataka kuondoka nalo na tayari wametoa maelekezo litakavyotekelezwa ni kuondokana na machinjio ambayo hayana majengo ya kudumu na kujenga machinjio mapya ambayo yanakidhi vigezo vya machinjio.
Alisema wamewaelekeza wamiliki kwenda kuchukua ramani zilizopo kwenye bodi ya nyama na kupeleka mkakati wa ujenzi wa machinjio mapya.
“Kwenye huu mkakati mpya tumepania kuboresha pia machinjio ya nguruwe na kuku yale ambayo hayako kwenye viwango tunataka machinjio yetu yawe na majengo yenye viwango vya kimataifa,” alisema Dk. Mwanga
Aidha, Dk. Mwanga alisema tangu waanze ukaguzi huo tayari wamefungia machinjio ya Ng’ombe ya Sabasaba iliyoko Mbagala Zakhem na machinjio ya nyama ya nguruwe sita yaliyoko katika Wilaya ya Ilala na Temeke.
Alisema machinjio ya ng’ombe Mbagala wameyafungia kutokana na hali ya uchafu na ukiukwaji wa uendeshaji wa machinjio ikiwa ni pamoja na uuzwaji wa wanyama ndani ya machinjo na miundombinu mibovu.
“Katika wilaya ya Temeke tumefungia machinjio ya nguruwe tatu na Ilala tumefungia tatu kwa sababu hakuna majengo ya kudumu, mazingira kuwa machafu, kutokuwa na miundombinu ambayo ni muhimu katika uendeshaji wa machinjio,” alisemaAlisema katika machinjio ya Pugu na Mazizini yaliyopo katika Wilaya ya Ilala walifanya ukaguzi jana saa 6:30 usiku na walibaini mambo mbalimbali ikiwamo biashara ya nyama ndani ya machinjio.
“Tatizo lingine ni uwepo wa watu wengi ndani ya machinjio," alisema.
"Kimsingi hawatakiwi kuwapo katika machinjio lakini wapo, yaani hakuna udhibiti wa watu kuingia katika machinjio na kivutio chao ni biashara ya nyama inayofanyika kinyume na taratibu.”
Alisema hali ya usafi katika machinjo hayo hairidhishi na jambo hilo limechangiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

No comments:

Post a Comment