Thursday, May 25, 2017

FEDHA ZA MCHANGA WA MADINI ZINGEWEZA KUJENGA RELI YA KISASA DAR-BUKOBA MARA 30


Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ambaye alikuwa akirejea kile kilichomo kwenye ripoti ya kamati hiyo, kwa wastani, kila mwezi taifa husafirisha mchanga wa dhahabu wa kati ya makontena 250 hadi 300 ya uzito wa wastani wa tani 20 kila moja.
Kwa kuzingatia, kiwango cha dhahabu kilichobainika kuwamo ndani ya kila kontena, dhahabu safi ya uzito wa zaidi ya tani 15 huwamo kwenye jumla ya makontena 277, sawa na ujazo wa madini hayo kwenye malori mawili aina ya Fuso yenye uzito wa tani 7 kila moja na tani nyingine moja ya kubebwa na gari ndogo ya mizigo (pick-up), kama ya aina ya Land Rover.
Aidha, kwa mujibu wa ripoti ya kamati, kwa ujumla thamani ya madini yote katika makinikia kwenye makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini, ni Sh. bilioni 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na Sh. trilioni 1.44 kwa kutumia viwango vya juu.
Kwa sababu hiyo, kama makontena 277 yaliyoshikiliwa kwa sasa yatachukuliwa kuwa ndiyo wastani wa makontena yanayosafirishwa kila mwezi (uhalisia wa idadi iliyoelezwa ni kati ya 250 hadi 350 kwa mwezi), maana yake thamani ya jumla kwa kutumia viwango vya juu kwa kipindi cha mwaka mmoja ni takribani Sh. trilioni 17.3.
Hivyo, kwa wastani huo, thamani ya madini yote yaliyosafirishwa kwa kipindi cha miaka 17 iliyopita ni sawa na takribani Sh. trilioni 294.
TRI. 294/- HUFANYA NINI?
Katika sehemu mojawapo ya hotuba yake baada ya kupokea ripoti ya kamati ya kuchunguza mchanga wa dhahabu jana, Rais Magufuli alisema taifa lingekuwa makini katika eneo hilo kwa miaka yote 17 na kuepuka upotevu wa mapato yake, hivi sasa Tanzania ingestahili kuwa miongoni mwa mataifa tajiri yanayotoa misaada (donor country) na siyo maskini kama ilivyo sasa.
Uchambuzi wa Nipashe, hasa kwa kutumia makadirio ya Sh. trilioni 294 zilizopotea katika miaka 17 iliyopita, unaonyesha kuwa ni kweli Tanzania ingekuwa mbali.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa, katika bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika mwezi ujao, serikali ilipanga kutumia Sh. trilioni 29.5. Hivyo, thamani yote ya mchanga wa madini ingeweza kukidhi bajeti sawa na ya mwaka huu wa fedha kwa vipindi vya takribani miaka 10.
Aidha, katika kipindi hicho cha miaka 17, fedha hizo za mchanga wa dhahabu Sh. trilioni 294 zingetosha pia kujenga zahanati za kisasa milioni 1.5 ikiwa kila moja ingejengwa kwa Sh. milioni 200, kununua madawati bilioni 2.1 kwa makadirio ya kila dawati kununuliwa kwa Sh. 140,000 na pia kuchimba visima virefu vya maji milioni 5.9 ikiwa kila kisima kitagharimu Sh. milioni 50.

Aidha, mchanganuo wa fedha za thamani hiyo (Sh. trilioni 294) unaonyesha kuwa zingeweza pia kuwapa mikopo wanafunzi milioni 11.5 kwa mwaka wa vyuo vya elimu ya juu katika miaka yote 17 ikiwa kila mmoja wao angepatiwa Sh. milioni 1.5.

Kiasi hicho cha fedha (Sh. trilioni 294) za thamani ya mchanga wa dhahabu kwa miaka 17 iliyopita kingetosha pia kujenga viwanja safi vya soka kama Uwanja wa Taifa vya idadi ya 5,250 ikiwa kila kimoja kingegharimu Sh. bilioni 56, sawa na kiasi kilichotumiwa na serikali za awamu ya Rais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kuukamilisha uwanja huo.
Kama hiyo haitoshi, thamani kubwa ya kiasi hicho cha fedha (Sh. trilioni 294) kinathibitishwa na mchanganuo mwingine kuhusu matumizi ya kila siku kwa ajili ya chakula. Ikiwa idadi ya Watanzania ni milioni 50, na ikiwa kila mmoja atapatiwa kiwango sawa cha Sh. 12,000 ili agharimie chai na silesi mbili za mkate wenye siagi pamoja na mlo mmoja wa wali nyama, maana yake fedha hizo (Sh. trilioni 294), zinaweza kuwalisha Watanzania wote chai na wali nyama kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne.
RELI KISASA, DAR BUKOBA MARA 30
Aprili 12 mwaka huu, Rais Magufuli alizindua awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa maarufu kama “standard gauge”, yenye urefu kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro huku thamani yake ikiwa ni Sh. trilioni 2.7.
Hivyo, ikiwa fedha za thamani ya madini yanayokadiriwa kuwamo kwenye mchanga wa dhahabu uliosafirishwa kwenda ughaibuni kwa miaka 17 zingetumika kujenga reli hii, maana yake zingekamilisha miradi 108 ya aina hiyo nchini kote, sawa na umbali wa kilomita 32,666.
Aidha, katika uchambuzi wake, Nipashe imebaini kuwa noti bilioni 29.4 za Sh. 10,000 zinahitajika kukamilisha kiasi cha Sh. trilioni 294. Noti hizo zinaweza kupangwa kwa urefu katika barabara itokayo jijini Dar es Salaam hadi Bukoba yenye urefu unaokadiriwa kuwa kilomita 1,379 (kwa kikokotozi cha distancefrom.com) na bado kiasi kingine kitabaki kwa kiasi cha mara 29.
Hesabu hizo zinatokana na ukweli kuwa kwa uchambuzi wa Nipashe, urefu wa noti moja ya sh. 10,000 ni sawa na sentimita 14.1, hivyo kwa noti bilioni 29.4, umbali wake kwa kuzitandaza ni sawa na sentimita 414,540,000,000 au kilomita 4,145,400 (kilomita moja ni sawa na sentimita 100,000).
Hivyo, noti hizo zikitandazwa barabarani ni sawa na kutembea safari 30 za kutoka Dar hadi Bukoba.

No comments:

Post a Comment