Thursday, April 27, 2017

YANGA KUIVAA MBAO BILA NYOTA WAKE HAWA WATATU


KIKOSI cha mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la FA, Yanga, kinatarajia kuondoka Dar es Salaam leo mchana kuelekea Mwanza kuwavaa wenyeji wao Mbao FC katika mechi ya hatua ya nusu fainali itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo, imeelezwa.

Yanga itaondoka jijini bila ya nyota wake watatu ambao ni washambuliaji Donald Ngoma, Malimi Busungu na beki Vincent Bossou.

Ngoma na Bossou hawakuwapo kwenye kikosi cha timu hiyo katika mechi iliyopita ya robo fainali ya Kombe la FA kutokana na kuwa majeruhi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema wachezaji wengine waliobaki wote wataondoka wakiwa na lengo moja la kwenda kusaka ushindi katika mchezo huo wa nusu fainali.

Saleh alisema wamejipanga kutetea ubingwa wa kombe hilo kwa sababu wanataka kuendelea kushiriki tena mashindano ya kimataifa hapo mwakani.

"Tunaondoka mchana, lakini wachezaji watatu hawataenda, Ngoma na Bossou hawajapona sawa sawa, Busungu yeye ana matatizo ya kifamilia," alisema meneja huyo.

Kocha wa timu hiyo Mzambia George Lwandamina alisema juzi kuwa pia vijana wake wako tayari kwa mechi hiyo ya Jumapili na nyingine tano za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizobakia ambazo nne watacheza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na moja ikifanyika ugenini Mwanza.

Mzambia huyo alisema mechi zote ni ngumu na kamwe hawatawadharau wapinzani wao kwa sababu hatua waliyofikia sasa ni yenye ushindani na changamoto mbalimbali.

Mbali na mechi hiyo, Jumamosi Simba watavaana na Azam FC katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini na bingwa wa michuano hiyo atakata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho A
frika.

No comments:

Post a Comment