Thursday, April 27, 2017

WALIMU WAMPASULIA YA MOYONIPROF. NDALICHAKO


WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA MAFUNZO YA UFUNDI, PROF. JOYCE NDALICHAKO.

WALIMU nchini wamemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, kutatua tatizo la uhaba wa walimu katika maeneo mbalimbali nchini, kwani wamekuwa wakifundisha vipindi vingi hivyo kujikuta wakirudi nyumbani wamechoka.

Walimu hao walisema hayo kwenye risala yao waliyoisoma mbele ya waziri huyo katika ufungaji wa mafunzo ya walimu wanaofundisha darasa la tatu na nne juu ya mtaala mpya unaozingatia ukuzaji wa umahiri wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), mjini hapa juzi.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na kuratibiwa na Wakala wa Usimamizi wa Elimu (ADEM).

Akisoma risala hiyo kwa niaba ya walimu wenzake wa wilaya za Bahi, Kondoa na Dodoma mjini, Eda Chilimo, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni kufundisha vipindi vingi kutokana na uhaba wa walimu.

"Mheshimiwa waziri pamoja na yote hayo tuliyokwambia, lakini changamoto kubwa ni upungufu wa walimu, tunafundisha vipindi vingi kiasi tukirudi nyumbani tunakuwa tumechoka sana, tunakuomba hili ulishughulikie,’’ alisema.

Alisema walimu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi na miundombinu kutokuwa rafiki kwa walimu na wanafunzi.

Akijibu risala hiyo, Prof. Ndalichako alikiri kuwapo na uhaba wa walimu na kuahidi kulitatua tatizo hilo kwa kuwaondoa walimu kwenye shule zenye ziada na kuwapeleka kwenye uhaba.

“Nakiri kweli hili ni tatizo, lakini kuna shule walimu wanagawana ‘topic’ katika somo moja, wakati nyingine hakuna walimu, hili halikubaliki ila kitaifa unaweza ukaona kama hakuna tatizo lakini ni tatizo,” alisema.

Waziri huyo aliwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nchini kuangalia jinsi ya kusawazisha ikama ya walimu katika maeneo yao.

“Ila na nyie walimu timizeni wajibu wenu, wengine wanafika kazini lakini hawatimizi wajibu wao tena hawaingii darasani mnashinda kutwa nzima katika ‘whatsup’ mkingalia shilawadu, sitaki tufike huko nawasihi tufanyekazi,’’ alisema.

Kuhusu ujenzi wa madarasa, alisema serikai imejenga madarasa 1,089, huku ikikarabati shule kongwe 88, lengo likiwa ni kuendeleza elimu nchini.

Aliwataka walimu hao kutowanyima wanafunzi vitabu vilivyotolewa na serikali kwani lengo ni wanafunzi wajue kwa ufasaha kusoma, kuandika na kuhesabu.

No comments:

Post a Comment