Na Omary Mngindo, Kibaha, Pwani, Tanzania- Aprili 23
WAKALA wa Ujenzi wa Barabara nchini Tanzania TANROAD'S Mkoa wa Pwani umewaondoa hofu wakazi ambao watapitiwa na mradi wa ujenzi wa Barabara inayotoka daraja la Makofia Bagamoyo mpaka Mlandizi.
Meneja wa Wakala hao Mkoani hapa Mhandisi Didas Msangi aliyasema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha muda mfupi baada ya kumalizika kwa Kikao cha Bodi ya Barabara kilichoketi chini ya Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo kilichojadili maendeleo ya barabara zilizomo humo.
Alisema kuwa Wakala hao tayari wameshafanya dizaini ya barabara inayotokea Bunju mpakani mwa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani itayoelekea Bagamoyo ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa upana wa njia nne.
"Itaanzia Bunju, Bagamoyo, Makofia mpaka Mlandizi kwa njia nne, tathimini kwa wananchi maeneo yatayohusika unaendelea, awali ilikuwa ya njia mbili, lakini sasa tumeongezeka upana itakuwa njia nne itaishia Mlandizi, baada ya hapo kuelekea Mzega wilaya ya Kisarawe itabaki ya njia mbili," alisema Mhandisi Msangi.
Aliongeza kuwa barabara hiyo ikifika mlima wa Dawasa unaopita kando ya Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Ruvu itaingia zaidi upande wa kulia hivyo kuiacha ya zamani ambayo itakwenda kutokea eneo ambalo kwa sasa lipo jengo la ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Vijijini.
"Mpango huo umelenga kuikwepa kona ambayo ipo jirani la ofisi za Dawasco ambayo kutokana na namna palivyo ingekuwa na ugumu wa kuipunguza, na kwamba lengo ni kuhepusha kutokea kwa ajali kutokana na eneo hilo kuwa na kona kali," alisema Meneja huyo.
Alieleza kuwa ujenzi huo utaanza mara baada ya kupatikana kwa fedha za fidia sanjali na za ujenzi na kuwa itakapokaribia wananchi watapewa tarifa mapema ili nao waweze kuwa na muda wa kutosha wa kuondoka kwenye maeneo husika kipisha zoezi litalotanguliwa na ulipwaji wa fidia.
Aidha Mhandisi Msangi alisema, kwa msimu wa bajeti ya mwaka 2017/2018 wametenga kiasi cha sh. Bil. 21.406, kati ya hizo sh. Bil. 10.235 kwa ajili ya Barabara Kuu, Bil. 11.170 kwa barabara za Mkoa, fedha za Maendeleo kutoka Serikali Kuu wameomba sh. Bil. 7.2 wakati mfuko wa Barabara wameomba sh. Bil. 5.48.
No comments:
Post a Comment