Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa
Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameitaka Serikali ieleze sababu za kuwatumbua watumishi bila ya kuwapa nafasi ya kujitetea.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Angella Kairuki alikana madai hayo akisema hakuna mtu anayetumbuliwa bila ya kufuata utaratibu.
Katika swali la nyongeza, Msigwa alitaka kujua haki za watumishi wanaotumbuliwa kwa kile alichokiita kwa mafungu, lakini bila ya kuwapa nafasi ya kujitetea.
Pia, alihoji wanatakiwa kutafuta haki yao wapi hata kama wametumbuliwa na Rais.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Ruth Mollel alitaka kujua ikiwa Tanzania inaongozwa kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni ni kwanini baadhi ya watumishi walioajiriwa wamekuwa wakisimamishwa kazi na Rais, wakuu wa mikoa na wilaya bila ya kuzingatia sheria ya utumishi wa umma na kanuni zake.
Akijibu, Waziri alisema kanuni za utumishi wa umma hutekelezwa kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni, utaratibu na miongozo na kwa mujibu wa ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kuhusu usimamizi na uendeshaji wa utumishi wa umma.
Alisema ibara ya Katiba imempa uwezo Rais wa kukasimu madaraka mbalimbali kwa ndani ya utumishi lakini kukasimu huko hakuwezi kutafsiriwa kuwa Rais hana mamlaka hayo tena kama ilivyofafanuliwa katika ibara 36 (4) ya Katiba na Kifungu cha 21 (4) na Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298.
Kairuki alisema hata watumishi waliofukuzwa au kusimamishwa kazi na Rais, wana nafasi ya kukata rufaa kwa mamlaka zingine na ikibainika kuwa walionewa, watapewa haki yao.
Katika majibu ya nyongeza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Tamisemi, George Simbachawene alisema wakuu wa mikoa na wilaya wanayo mamlaka lakini wanapotoa uamuzi wa kuwasimamisha kazi watumishi, huwa si mwisho bali wakurugenzi ndiyo hutakiwa kuchukua hatua au makatibu tawala wa mikoa.
No comments:
Post a Comment