Tuesday, March 21, 2017

YANGA YAICHOMOLEA POLISI DODOMA


BAADA ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zanaco, uongozi wa Yanga umesema hautacheza tena mchezo wa kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma na nguvu sasa watazielekeza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilikubali kwenda Dodoma kucheza mechi hiyo ya kirafiki Machi 25,mwaka huu na hiyo ilikuwa ni kuwapa nafasi mashabiki wao kukiona kikosi cha timu hiyo baada ya mahasimu wao Simba kufanya hivyo hivi karibuni.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema wameamua kubadili uamuzi wa kwenda Dodoma kutokana na majukumu ya kutetea ubingwa na kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Shirikisho waliyohamia.

Mkwasa alisema pia kutofahamu mpinzani watakayekutana naye ni jambo lingine lililosababisha kubadili uamuzi walioufanya hapo awali baada ya kupokea mwaliko kutoka katika Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (Dorefa).

"Ratiba ya timu imezidi kutubana, hatutaki kuwaambia waendelee na maandalizi halafu tukapeleka Timu B, tutakuwa hatujawatendea haki mashabiki wetu, tutaangalia nafasi nyingine itakapopatikana ndiyo tutaenda Dodoma, watusamehe," alisema Mkwasa.

Katibu huyo alitaja sababu nyingine ambayo imefanya wasiende kucheza mechi hiyo ni wachezaji wake waliokuwa majeruhi bado hali zao hazijaimarika vema.

Mapema mwezi huu Dorefa iliwaalika Simba kucheza na 'Maafande' hao na vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

No comments:

Post a Comment