Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana katika
Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga ameingia matatani tena
baada ya Mahakama Kuu kuamuru akamatwe na kufikishwa mahakamani hapo.
Amri hiyo ilitolewa na Naibu Msajili wa Wilaya, Mahakama Kuu, Ruth
Masambu wiki iliyopita baada ya Dk Mahanga kushindwa kufika mahakamani
hapo bila taarifa.
Dk Mahanga ambaye alikuwa mbunge wa Ukonga na baadaye Segerea kwa tiketi
ya CCM, alitakiwa kufika mahakamani hapo Alhamisi iliyopita ili kulipa
Sh2 milioni, ikiwa ni sehemu ya deni la zaidi ya Sh11 milioni
anazodaiwa.
Mwanasiasa huyo ambaye sasa ni kada wa Chadema, anadaiwa kiasi hicho na
mwanaharakati wa haki za binadamu, Kainerugaba Msemakweli ikiwa ni
gharama alizozitumia katika kesi ya madai ya kashfa iliyofunguliwa dhidi
yake na Dk Mahanga.
Dk Mahanga alifungua kesi ya madai namba 145 ya mwaka 2009 akidai kuwa
kitabu alichoandika mwanaharakati huyo cha “Orodha ya Mafisadi wa Elimu
Tanzania” kikimtaja kuwa ni mmoja wa vigogo wenye shahada za udaktari wa
falsafa za kughushi, kilimdhalilisha.
Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa Julai Mosi, 2014 kutokana na Mahanga na mawakili wake kutofika mahakamani mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment