Wednesday, March 15, 2017

WALIOACHA BANGI WATAKA WATUMIKE KUELIMISHA JAMII

Vijana 10 waliokuwa wakijihusisha na uvutaji wa bangi katika Kata ya Ipagala, Manispaa ya Dodoma wamejisalimisha katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata na kusema wameacha na wanataka watumike kama walimu kuelezea madhara ya tabia.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ipagala, Khalifa Malaja, alisema baada ya kujisalimisha vijana hao walihojiwa kuithibitishia Ofisi hiyo na jamii inayowazunguka kuwa watakuwa mabalozi wazuri kwa vijana wenzao nao waache.

Kwa mujibu wa Malaja, vijana hao wameomba jamii iwatambue kuwa wamedhamiria kufanya mabadiliko chanya na kwamba, watashirikiana na raia wa eneo kuendeleza ujenzi wa taifa na kuwafichua wauzaji wa bangi.

Ofisa Mtendaji huyo aliwapongeza vijana hao kwa kile alichokiita kuwa ni ushujaa waliofanya. Aliwataka vijana wengine kuiga mfano huo ili kuisaidia Serikali kufanikisha mapambano dhidi ya dawa zote za kulevya ikiwamo bangi na kulinda nguvu kazi ya taifa.

Aliwataka waunde kikundi cha ujasiriamali ili wakidhi vigezo vya kupata mikopo itakayowasaidia kuendesha biashara na kujikwamua kiuchumi. Malaja alisema anaamini baada ya vijana hao kukiri, jamii itafuatilia mwenendo wao na kuwa tayari kushirikiana nao.

No comments:

Post a Comment