Saturday, March 18, 2017

SUMATRA YATISHWA ZIGO LA LAWAMA


DALADALA ZINAZOFANYA SAFARI ZAKE NDANI YA MANISPAA YA DODOMA.

WAMILIKI  wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake ndani ya manispaa ya Dodoma, maarufu kama daladala na wale wa magari yanayofanya safari kati ya Majengo na Nala,

Wameilalamikia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoani humo kwa madai ya kuomba rushwa na kuwapa faini kubwa kwa makosa ‘bubu’.

Malalamiko hayo yalitolewa jana na wamiliki hao na madereva baada ya kwenda kueleza kero zao ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, kutokama na magari yao kuzuiwa na Sumatra kwa madai kuwa yalifanya makosa ya kubadili ruti bila kibali.

Mmoja wa wamiliki hao, James Minja, alisema magari yao yalikamatwa juzi na mamlaka hiyo kwa madai yalifanya makosa, lakini bila kuwaeleza makosa hayo kisha kulazimishwa kulipa faini ya Sh. 120,000 kwa kila gari lililokamatwa.

Minja alisema pamoja na Sumatra kuwaamuru walipe kiasi hicho cha fedha, polisi walishindwa kubaini makosa ambayo yalitakiwa kulipiwa kiasi hicho cha fedha hali ambayo kikosi cha usalama barabarani kiliamua magari hayo yalipiwe faini ya Sh. 60,000 kila moja.

“Tumekamatwa na kupelekwa pale lakini cha ajabu hata makosa walishindwa kutueleza hata polisi wenyewe wameshindwa kutuandikia makosa ya Sh.120,000, hali ambayo walibidi kubuni makosa na kutuandikia tulipe 60,000,” alisema Minja.

Alisema pamoja na polisi kuwalipisha Sh. 60,000, walipokwenda katika ofisi za Sumatra na kuonyesha stakabadhi za malipo ili wapatiwe vibali vyao vya safari walikataliwa na kuambiwa wanatakiwa kulipa Sh. 120,000 ndipo wapatiwe.

“Kutokana na kutaka kuondoa usumbufu ili tuendelea na kazi tuliamua kulipa kiasi hicho cha fedha na tulirudi polisi na kutaka kumaliza kiasi hicho kilichobakia cha Sh. 60,000, lakini polisi walikataa na kutueleza faini yao ilikuwa 60,000 na sio 120,000 kama ambavyo Sumatra wanataka,” alisema Minja.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, alisema aliyapokea malalamiko hayo tayari na amewasiliana na mkuu wa usalama barabarani mkoani humo, ili kuhakikisha anayafanyia kazi haraka na kuwachukulia hatua kali watakaohusika kukiuka kanuni na sheria za nchi.

“Nimepatiwa malalamiko mengi sana ambayo mengine siwezi kuyaweka wazi hapa kwakuwa inabidi hivi sasa hata vyombo vyetu vishirikishwe katika maamuzi lakini pia mimi kama mkuu wa wilaya nitachukua hatua kali kwa yoyote yule atakaye bainika na magari yaliyokamatwa yanatakiwa kuachiwa kwa kuwa kilichokuwa kinadaiwa kimelipwa,” alisema Mndeme.

Meneja Mfawidhi wa Sumatra mkoani Dodoma, Conrad Shio, alisema magari hayo yaliyokamatwa yalitakiwa kulipa Sh. 120,000 kama faini na Sh. 60,000 kutokana na kuegeshwa na kufanya kituo eneo lililokatazwa na serikali ya mkoa.

“Pale walipokamatwa ni eneo ambalo hawatakiwi kuweka stendi lakini wao niliwakuta wakiwa wamepaki katika eneo lile ambalo ni kwajili ya kushusha na kupakia tu lakini nashangaa polisi wakasema kuwa wamewalipisha Sh. 60,000 badala ya Sh. 120,000 kimakosa,” alisema Shio.

No comments:

Post a Comment