Ivanka Trump amejiunga rasmi na serikali ya babake ambapo atahudumu kama
mfanyakazi asiyelipwa, kwa mujibu wa Ikulu ya White House.
Cheo chake halisi kitakuwa Msaidizi wa Rais.
Binti huyo wa Rais wa Marekani amekubali shinikizo baada ya wataalamu
kuhusu maadili kukosoa mpango wake wa awali wa kutaka kuhudumu katika
wadhifa usio rasmi.
Bi Trump, 35, amesema amesikia "maswali ambayo baadhi ya watu wamekuwa
wakiuliza kuhusu hatua yangu kumshauri Rais katika nafasi yangu kama mtu
binafsi".
Mumewe, Jared Kushner, ni mshauri mwandamizi wa Rais Donald Trump.
Kupitia taarifa, White House imesema ina furaha kwamba "Ivanka Trump
amechukua hatua hii isiyotarajiwa katika nafasi yake kama binti wa Rais".
Bi Trump alisema kupitia taarifa yake kwamba amekuwa akifanya kazi "kwa
nia jema na kundi la washauri wa rais White House pamoja na mshauri wake
binafsi kujadili kuhusu jukumu lake".
Wataalamu kuhusu maadili walilalamika ilipobainika wiki iliyopita kwamba
Bi Trump angepewa afisi White House pamoja na kibali cha usalama cha
kuingia na kuondoka ikulu hiyo, bila yeye kujiunga rasmi na wahudumu wa
rais.
Wakosoaji walisema kazi ya Bi Trump inafaa kufanywa rasmi ndipo aweze
kudhibitiwa na sheria kuhusu uwazi wa maafisa wa serikali pamoja na
maadili. Aidha, adhibitiwe na sheria kuhusu mgongano wa maslahi.
Wakili wa Bi Trump, Jamie Gorelick, amesema mteja wake atawasilisha
nyaraka zifaazo za kufichua utajiri wake kwa mujibu wa sheria kuhusu
maadili ya watumishi wa umma Marekani.
No comments:
Post a Comment