Tuesday, March 14, 2017

MAHAKAMA YAMBANA MDEE KWA UDHURU

MBUNGE WA KAWE, HALIMA MDEE.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuonya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kutoa udhuru kwa kufuata taratibu za kisheria badala ya kutofika mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili bila ruhusa.

Aidha, mahakama hiyo, imemweleza mbunge huyo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kadi zake za onyo sasa zimekwisha.

Mdee pamoja na wabunge wengine wawili wa Chadema, Mwita Waitara, Saed Kubenea pamoja na wenzao wawili, wanakabiliwa na mashtaka ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando.

Akitoa onyo hilo, Hakimu Shaidi alisema: "Sasa ni mara ya pili Mdee kusafiri nje ya nchi bila kufika mahakamani pasipo kutoa taarifa na kusababisha kesi hii kusimama kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri."

“Mara ya kwanza, wenzako walisema umekwenda Kenya kwenye michezo ya kibunge bila ruhusa wala taarifa kutoka kwa mawakili wako…wiki iliyopita, umesafiri kwenda Marekani bila kibali cha mahakama. Kadi zako za onyo zimekwisha.”

“Kati ya Mahakama na Bunge, nadhani Mahakama ni muhimu kuliko hilo Bunge. Kwa hiyo fuata taratibu za kisheria, usikwamishe kesi kuendelea.”

Hata hivyo, Mdee alidai kwamba alimjulisha wakili wake kuhusu safari pamoja na barua ya ruhusa na kuionyesha mahakama hiyo nyaraka za safari ikiwamo tiketi na viza.

Wakili wa utetezi, Hekima Mwesiga, alidai kuwa ni kweli mshtakiwa aliacha nyaraka, lakini kwa bahati mbaya alikuwa nazo Wakili Peter Kibatala katika kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

“Tutaonana wabaya katika hili, ni lazima unapofanya kitu taratibu zifuatwe kuwe na nidhamu,” alisisitiza Hakimu.

Awali, upande wa Jamhuri ulikuwa na shahidi mmoja, Mrakibu wa Polisi (SP) Euegin Mwampondele, ambaye alidai kuwa siku ya tukio alimwona mshtakiwa wa kwanza, Rafii Juma na Mdee, wakimkwida Mmbando na kufanikisha kuporwa nyaraka za kusitisha uchaguzi.

Pia, alidai kuwa mshtakiwa Waitara, alishika kipaza sauti na kuwatangazia wajumbe wa mkutano huo kugoma kuondoka katika ukumbi huo.

“Watu walisogea na kumzonga Mmbando na kuanza kumshambulia, ndipo mimi nikishirikiana na askari watatu, tulipomtoa kupitia mlango maalum, lakini alishajeruhiwa,” alidai shahidi huyo.

Mbali na wabunge hao na Juma, washtakiwa wengine ni Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (56) na Diwani wa Kata ya Saranga Kimara, Ephreim Kinyafu (33).

Washtakiwa wanadaiwa kuwa Februari 27, mwaka 2016 katika Ukumbi wa Karimjee Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha mwilini.

Tukio hilo linadaiwa kutokea siku ya uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam na Naibu Meya wake.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo.

No comments:

Post a Comment