Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
ameagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya
ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India
Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo
itakapokamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao
ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 03 Machi, 2017 alipotembelea
mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5
za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa
na tatizo kubwa la maji.
Mhe.
Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo
ambao tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 21.8 zimetolewa kati ya Shilingi
Bilioni 29 zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake, na ameonya kuwa
endapo mradi huo hautakamilika katika kipindi cha miezi 4 kuanzia sasa
atachukua hatua dhidi ya wanaopaswa kuusimamia.
"Ikipita
miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wanashida
ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India,
mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo
la ujenzi halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria
zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Mapema
akitoa maelezo kuhusu mradi huo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi
Gerson Lwenge amesema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambapo hadi sasa
umefikia asilimia 85 na kwamba mkandarasi amesimamisha kazi kutokana na
kuishiwa fedha.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya
Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ameiomba bodi hiyo
ishirikiane na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji wa
umeme na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa "Standard Gauge".
Pamoja
na kutoa ombi hilo Mhe. Dkt. Magufuli ameipongeza benki hiyo kwa kutoa
mikopo nafuu iliyowezesha kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo hapa
nchini hususani ujenzi wa barabara lakini ameomba mchakato wa
upatikanaji wa mikopo hiyo urahisishwe na kuharakishwa ili miradi mingi
zaidi itekelezwe kwa wakati.
"Hapa
Tanzania AfDB imefanya mambo makubwa sana, tunaipenda sana benki hii
kwa sababu imetuwezesha kujenga barabara nyingi zikiwemo ya Iringa -
Dodoma inayounganisha Cape Town Afrika Kusini hadi Misri, barabara ya
Namtumbo - Tunduru - Masasi na nyingine nyingi, kwa kweli hawa ni wadau
muhimu wa maendeleo" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza
baada ya kikao hicho kiongozi wa Bodi ya Wakurugenzi waliokutana na
Mhe. Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Lindi Bi. Lekhethe Mmakgoshi
amempongeza Mhe. Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuleta mageuzi ya
kiuchumi nchini Tanzania na ameahidi kuwaAfDB itaendelea kuwa mshirika
muhimu wa maendeleo ya Tanzania ikiwemo kufanyia kazi maombi aliyoyatoa
kwa Bodi hiyo.
Nae
Dkt. Namajeje Weggoro ambaye ni mmoja wa wakurugenzi hao anayewakilisha
nchi saba za Afrika ikiwemo Tanzania amesema Tanzania ni nchi
inayoongoza kwa kupata mikopo mingi kutoka AfDB na ameongeza kuwa maombi
yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli yatapewa kipaumbele.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
03 Machi, 2017
No comments:
Post a Comment