WATU wanne wamefikishwa mahakamani katika kesi mbili tofauti za uhujumu
uchumi, kwa kuingiza nchini magari sita kwa kuficha na nguo za mitumba,
maarufu kama makontena ya Magufuli, na kuisababishia serikali hasara ya
kukosa mapato ya Sh. milioni 478.7.
Katika kesi ya kwanza, watu wawili akiwamo raia wa Zambia, Agustino
Kalumba (36) wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka matatu ya
kula njama, uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya kukosa
ushuru wa Sh. milioni 287.8.
Mbali na Kalumba mshtakiwa mwingine ni, Sultan Hassan (29) maarufu kama Mwarabu.
Washtakiwa walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga akisaidiana na Wakili wa Serikali Batilda Mushi.
Katuga alidai kati ya Desemba mosi, mwaka jana na Machi mosi washtakiwa
wakiwa na wengine ambao hawapo mahakamani walikula njama ya kutenda kosa
la kusafirisha mali iliyofichwa.
Katika shtaka la pili, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya
Desemba mosi na 31, mwaka jana katika Bandari ya Dar es Salaam, iliyopo
Temeke jijini Dar es Salaam, waliingiza gari tatu aina ya Range Rover
Sports za rangi nyeusi, nyeupe na 'daki bluu'.
Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa gari hizo ziliambatana na nguo, mabegi
na viatu vya mitumba wakiwa na lengo la kuwadanganya maofisa watoza
ushuru.
Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa kati ya Desemba mosi, mwaka jana na
Machi mosi katika bandari hiyo, washtakiwa waliingiza mali wakiwa
wameficha na kuisababishia serikali kukosa mapato ya Sh. 287,801,825.19
iliyokuwa kwenye kontena namba MSKU 9914168.
Hakimu Simba aliwaeleza washtakiwa hao kwamba kesi inayowakabili ni
uhujumu uchumi, hivyo hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama
yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Katuga alidai kuwa upelelezi upo katika hatua za mwisho kwa ajili ya
kuchanganua kama kesi hiyo itasikiliza na mahakama hiyo au Mahakama
Maalumu ya Ufisadi.
Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 12 na washtakiwa wapelekwe mahabusu.
KESI NYINGINE
Katika kesi nyingine, Hassan na Ramadhani Hamis wamesomewa mashtaka
matatu ikiwamo kula njama, uhujumu uchumi na kuisababishia serikali
hasara ya Sh. milioni 190.9.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Katuga alidai kuwa Kati ya Desemba mosi, mwaka jana na Machi mosi
washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la kuingiza mzigo ukiwa
umefichwa.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Januari 24 katika Bandari ya Dar es Salaam, iliyoko Wilaya ya
Temeke, jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliingiza magari matatu aina
ya Range Rover Sports baada ya kuyaficha pamoja na nguo, viatu na
magodoro ya mitumba.
Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la tatu kuwa kati ya Desemba
mosi, mwaka jana na Machi 4, washtakiwa waliingiza nchini magari matatu
kwa kuficha na kuisababishia serikali kupata hasara ya sh.
190,923,267.76.
Katuga alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mwijage alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Alisema washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu hadi Aprili 12 kesi yao itakapotajwa.A
No comments:
Post a Comment