Hatimaye
gazeti la MAWIO lililofutwa na serikali ya Tanzania na kuacha
kuchapishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, limerejea mtaani kwa uamuzi wa
Mahakama Kuu.
Serikali ililifuta gazeti hilo na kulizuia kuchapishwa kwa njia yoyote ile Januari 15, mwaka jana- 2016.
Uamuzi
wa Mahakama Kuu uliotolewa Jumanne , umetupilia mbali amri ya serikali
ya “kuliua na kulizika kabisa” gazeti hilo lililokuwa likitoka kila wiki
– Siku ya Alhamisi.
Mahakaka Kuu ilisema kuwa amri ya serikali kuliua MAWIO haikuwa sahihi, hivyo “gazeti hilo lilionewa.”
Jopo
la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo, limesema gazeti
la MAWIO halikupewa nafasi ya kujitetea kabla ya hatua ya serikali ya
kulifuta kutoka orodha ya msajili wa magazeti nchini.
Msajili wa magazeti nchini ni Idara ya Habari Tanzania (MAELEZO).
Jaji
Ignas Kitusi ndiye alisoma uamuzi wa Mahakama kuu – kwa niaba ya jopo
siku ya Jumanne, wiki iliyopita (Februari 28). Jaji mwingine aliyekuwa
kwenye jopo hilo, ni Jaji Ama-Isario Munisi.
Serikali ililifuta gazeti la MAWIO tarehe 15 Januari 2016 baada ya kudaiwa kuandika ilichoita habari na makala za “kichochezi.”
Utawala
wa Kampuni ya Victoria Media Services Limited, wachapishaji wa gazeti
la MAWIO, uliamua kufungua kesi mahakamani. Hii ni kesi Na. 15 ya mwaka
2016.
Wakili
wa MAWIO, Dk. Rugemeleza Nshalla, amesema kuwa hatua ya serikali
iliegemea falsafa ya “…Nyonga kwanza na sikiliza baadaye.”
Dk.
Nshalla amesema katika mazingira yoyote yale, sharti walalamikiwa
wapate nafasi ya kujieleza na kusiklilizwa na mahakama kwanza kabla ya
hukumu kutolewa.
Mkurugenzi
Mtendaji na Mhariri Mkuu wa gazeti la MAWIO, Simon Mkina amesema
alishangazwa sana na hatua ya serikali kufuta alichoita “mdomo wa
wananchi.”
“Kufuta chombo hiki au kingine kama hiki, ni kukiri kuwa serikali haipendi kusikia kutoka kwa wananchi…” amesema Mkina
Mkina
amesema MAWIO limekuwa gazeti linalozingatia maadili na kufuata weledi
wa hali ya juu katika kuandika na kuchapisha habari na makala na
kuongeza kuwa limekuwa gazeti pekee linalotoa uwanja mpana kwa wananchi
kuandika mawazo yao ili kuchochea uwajibikaji wa viongozi wa serikali.
Mkina
amesema kufuatia uamuzi huo wa Mahakama Kuu, MAWIO litarejea mtaani
Alhamisi ya wiki hii na kuahidi kuwapa wasomaji wake habari
zilizofanyiwa kazi ya ziada.
“Kwa
muda wa zaidi ya mwaka mmoja, wakati gazeti halipo mtaani – likiwa
limefutwa na serikali, pamoja na kupoteza ajira za watu na kuingia
katika hasara kubwa, bado tulikuwa na kazi ya kujiuliza ni wapi
tulikosea na je, lini tutapewa haki yetu? Bahati nzuri haki yetu
imefika,” aliongeza Mkin.
Uamuzi
na hatua ya kulifuta MAWIO, lililokuwa likichapishwa kila Alhamisi,
ulitangazwa na Nape Nnauye, Waziri wa habari, vijana, utamaduni, sanaa
na michezo.
Tangazo
lililotolewa katika gazeti la serikali, Na. 55 la Januari 15, 2016,
lilisema serikali inachukua uamuzi wa kulifuta kwa mujibu wa mamlaka
iliyonayo kupitia Sheria ya Magazeti ya 1976; sura ya 229 kifungu cha
25(1).
No comments:
Post a Comment