Wafanyakazi
wengine wawili wa Kampuni ya Quality Group inayomilikiwa na Yusuf Manji
ambao ni raia wa India wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuzuia
maofisa wa Uhamiaji kutimiza majukumu yao.
Washitakiwa
hao ni Jose Kiran (40) ambaye ni Meneja Miradi wa kampuni na Prakash
Bhatt (35) ambaye ni Katibu Muhtasi wa kampuni hiyo ambao wameongezwa
katika kesi inayowakabili wafanyakazi 14 wa kampuni hiyo, raia wa India
wanaokabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la kughushi viza ya biashara.
Wakili
wa Serikali, Method Kagoma alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Cyprian Mkeha kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha
Kifungu Namba 30 (1) (f) na Kifungu Namba 2 cha Sheria ya Uhamiaji ya
Mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Namba 8 ya Mwaka 2015.
Kagoma
alidai washitakiwa hao wawili, Februari 20 mwaka huu katika Kampuni ya
Quality Group waliwazuia maofisa Uhamiaji kutimiza majukumu yao baada ya
kukataa kuripoti kwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa
kujaribu kukimbia nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mpaka
wa Horohoro.
Washitakiwa
wote walikana mashitaka ambapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo
upande wa mashitaka unaomba tarehe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya
awali.
Hata
hivyo, washitakiwa waliachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya
dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini
dhamana ya Sh milioni tano.
Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo itatajwa Machi 7 mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Mbali
na washitakiwa hao, wengine katika kesi hiyo ni Rajat Sarkar (35),
Jagadish Mamidu (29), Niladri Maiti (41) Divakar Raja (37) ambao ni
washauri wa kampuni hiyo, huku Mohammad Shaikh (44) mhasibu na Pintu
Kumar (28) ambaye ni Meneja msaidizi wa kampuni.
Pia
wapo ni Bijenda Kumar (43), Prasson Mallik (46), Nipun Bhatt (32), Anuj
Agarwal (46), Varun Boloor, Arun Kateel (46), Avinash Chandratiwari
(33) na Vikram Sankhala (50) ambao wote ni washauri wa kampuni hiyo.
Kagoma alidai katika mashitaka ya kwanza washitakiwa walitenda kosa hilo
Februari 13, mwaka huu maeneo ya Kampuni ya Quality Group, Ilala Mkoa
wa Dar es Salaam.
Alidai
kuwa washitakiwa wote wakiwa ni raia wa nchini India, walikutwa na visa
zilizoghushiwa kinyume na kifungu namba 31 (1) (e) na Kifungu Namba 2
cha Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho na sheria
namba 8 ya mwaka 2015. Kagoma alidai katika mashitaka ya pili kuwa
washitakiwa wote kwa pamoja katika tarehe hiyo hiyo, mwaka huu, maeneo
ya Kampuni ya Quality Group, walikutwa wakiishi nchini kinyume na
sheria.
Pia
katika mashitaka ya tatu, inadaiwa washitakiwa wakiwa katika Kampuni
hiyo, huku wakijua kuwa wao ni raia wa India walikutwa wakifanya kazi
nchini kinyume na kifungu namba 9 (i) (e) na kifungu namba 3 cha sheria
ya ajira namba 1 ya mwaka 2015.
Hivi
karibuni, Ofisi ya Uhamiaji ilitaja wafanyakazi 25 wa Yusuf Manji
kwamba wanafanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali na kukusudia
kumfungulia mashitaka mfanyabiashara huyo ambaye pia anakabiliwa na kesi
ya kutumia dawa za kulevya, kwa kosa la kuajiri wafanyakazi kutoka nje
ya nchi wasio na vibali.
No comments:
Post a Comment