Friday, February 24, 2017

SIMBA Vs YANGA VUTA NIKUVUTE KESHO


SIMBA na Yanga zinatarajiwa kukutana kesho katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, presha ni kubwa lakini kila upande umeshajihakikishia kuwa lazima wenyewe ndiyo uibuke na ushindi.

Suala la sare linaonekana kutotakiwa na pande zote, mchezo ukiisha kwa sare itakuwa mbaya kwa Simba kwa kuwa itaendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili lakini Yanga nayo itakuwa nyuma kwa tofauti ya pointi hizo na kutegemea mechi ya kiporo ambayo kama mambo yataenda vibaya basi itajiweka kwenye mazingira magumu.

Timu zote zimesaliwa na michezo michache kumaliza msimu, hivyo jambo pekee lenye faida kwao ni ushindi tu kwa kila mmoja ili kutengeneza mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa. Presha kubwa, kocha anena Kocha wa Yanga, George Lwandamina amebadili mbinu ili kukifanya kikosi chake kuwa imara katika kambi yao iliyopo Kigamboni jijini Dar.

Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo ni kuwa Lwandamina amekuwa akitoa mazoezi yenye mbinu tofauti na siku za nyuma kambini huko na wachezaji wamekuwa bize huku akiwataka kuongeza umakini.

KOCHA: ATAKAYESHINDA BINGWA

Kocha Mkuu wa Singida United, Fred Felix Minziro ambaye aliwahi kuwa kocha wa Yanga ameuzungumzia mechi hiyo kwa kusema ni fainali kutokana ndiyo itakayoonyesha mwanga wa nani atakuwa bingwa wa ligi msimu huu. “Mchezo utakuwa mgumu sana hivyo siwezi sema nani anaweza kuibuka na ushindi kwani linapokuja suala la mechi hii hakuna mbabe kwa mwenzake na kinachotokea ni bahati nasibu kwani timu yeyote inaweza kushinda,”  alisema Minziro.

MANARA ACHEZESHE

Licha ya Bodi ya Ligi Kuu Bara kuficha majina ya waamuzi, uongozi wa Yanga umesema kuwa wao hawana hofu na wangefurahi zaidi mechi yao ya watani wa jadi, basi ingechezeshwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi alisema kama Manara atakubali kuchezesha mechi hiyo, basi ni lazima achezeshe kwa kanuni 17 za soka.

“Kwetu hatuna hofu kabisa juu ya waamuzi watakaochezesha pambano hilo na kikubwa tunataka waamuzi wanaochezesha kwa haki kwa kutumia kanuni 17

za mchezo huo. “Sisi tupo tayari mechi hii dhidi ya Simba tuchezeshwe na Manara baada ya wao kukataa waamuzi hapa nyumbani na kutaka waamuzi wa nje ya nchi,” alisema.

MWANJALE FITI, KUKIPIGA

Habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kuwa beki wa kati Mzimbabwe, Method Mwanjale, juzi alianza program ya mazoezi magumu na wenzake chini Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog. Beki huyo alikuwa nje ya uwanja kwa wiki moja akiuguza majeraha ya enka aliyoyapata mechi ya Ligi Kuu Bara na Prisons kabla ya kutolewa nje kutibiwa.

Daktari Mkuu wa Simba, Yassin Gembe amesema tangu wameweka kambi Jumapili iliyopita beki huyo alikuwa ana program maalum ya binafsi kwa hofu ya kujitonyesha jeraha lake lakini tayari ameanza mazoezi magumu baada ya kumaliza program ya mazoezi mepesi ya binafsi.

KABURU AFUNGUKA

Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ameweka wazi kwamba kikosi chao kipo kamili na kina matumaini makubwa ya kushinda mechi hiyo kwa sababu ya maandalizi ambayo wameyafanya.

No comments:

Post a Comment