Wednesday, February 8, 2017

MAKONDA ATOA KAULI ZA DHARAU DHIDI YA BUNGE....AITWA BUNGENI KUJIELEZA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli moja limewaita mbele ya Kamati yake ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, na DC wa Arumeru Alexander Mnyeti kwa madai ya kudharau Bunge.

Maamuzi hayo ni sehemu ya maazimio manne ya  Bunge yaliyopishwa usiku huu dhidi ya viongo wanaoteuliwa na Rais hasa wakuu wa mikoa na wilaya, ambapo azimio lingine ni kumtaka Waziri wa TAMISEMI kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutoingilia majukumu yasiyo yao.

Hatua hiyo inafuatia hoja iliyotolewa bungeni hapo na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, kufuatia kauli inayodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa  Dar es Salaam Paul Makonda inayodaiwa kuwa ni dharau kwa Bunge.

Pia Mwita amedai kuwa viongozi mbalimbali hasa wakuu wa mikoa na wkuu wa wilaya wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kiasi cha kuingilia majukumu yasiyo yao, na wakati mwingine kuingilia majukumu ya Bunge, na kutolea mfano Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Alexander Mnyeti.

Baada ya hoja yake kukubaliwa na Mwenyekiti wa kikao hicho Mh Andrew Chenge, wabunge wameijadili ambapo wabunge kadhaa akiwemo Ester Bulaya, Zitto Kabwe, Saed Kubenea na Joseph Musukuma wamepata fursa ya kuchangia ambapo kwa kiasi kikubwa wote wameoneshwa kukerwa na  kauli hiyo inayodaiwa kutolewa na Paul Makonda, pamoja na utaratibu wa wabunge kukamatwa bila utaratibu.

Wakati mbunge Zitto Kabwe akipendekeza kuitwa mbele ya kamati viongozi waliotuhumiwa, Ester Bulaya amepasua jipu kwa kusoma ujumbe wa vitisho aliodai umetoka kwa kiongozi mmoja aliyeteuliwa na Rais.

Akichangia mjadala huo, Waziri anayehusika na Bunge pamoja na sera Mh. Jenista Mhagama amewataka wabunge kutomuhusisha Rais Magufuli na makosa yanayofanywa na viongozi aliowateua ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa sheria Rais ana majukumu yake, na wakuu wa mikoa na wilaya wana wajibu wao, hivyo kama kuna RC au DC anakwenda kinyume na sheria au kuingilia Bunge, anapaswa kuwajibishwa mwenye.

Baada ya mjadala huo, Chenge amewahoji wabunge wanaokubaliana na mapendekezo ya mtoa hoja, ambapo wabunge wote wameitikia kuunga mkono mapendekezo hayo manne na kuwa maazimio rasmi ya Bunge.

No comments:

Post a Comment