Chama
cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) kimemwandikia barua Waziri wa
Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe kikimtaka aache kuingilia
uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Barua
hiyo imekuja baada ya Dkt. Mwakyembe kudaiwa hivi karibuni kutishia
kuifuta TLS kwa madai kwamba imeanza kuingiliwa kisiasa.
Barua
hiyo iliyoandikwa na kusainiwa na Rais wa EALS, Richard Mugisha,
inasema TLS si chama cha kisiasa na kimeanzishwa kwa kufuata sheria
zote.
“Mheshimiwa
Waziri, tumesikitishwa na taarifa ambazo zimeenea kwenye vyombo vyote
vya habari na gazeti la East African la Februari 18 ambalo limekunukuu
ukisema kwamba Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kina muingiliano
wa kisiasa,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Katika
barua hiyo, Mugisha anasema wanasheria wanatakiwa wapewe uhuru,
wasiingiliwe na serikali kama ilivyo kwa nchi nyingine kwani kuingilia
ni sawa na kuvunja sheria za nchi.
Rais
wa sasa wa TLS, John Seka amesema kuwa chama chake kimefurahishwa na
barua hiyo kwa Waziri na kwamba nao pia wanafanya taratibu kumuona ili
kujadili mustakabali wa chama hicho.
Alisema
kuwa TLS inaendelea na mchakato wa uchaguzi kama ulivyopangwa na
kuwataka wagombea wote kujiandaa kwa uchaguzi huo ambao alisema ni
halali.
Uchaguzi
wa chama hicho unatarajiwa kufanyika machi 18 mwaka huu, huku wagombea
kutoka vyama vya upinzani wakiwa wamejitokeza kuwania nafasi ya uongozi
wa juu.
No comments:
Post a Comment