Friday, August 10, 2018

LUGOLA AITAKA TFF KUJIPANGA KATIKA HILI

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka utaratibu mzuri kwa waandishi wa habari kuweza kufanya kazi zao vyema wanapokuwa uwanjani bila kusuguana na vyombo vya ulinzi.

Lugola, alitoa kauli hiyo muda mchache kabla ya kuondoka kwenye Uwanja wa Taifa juzi alipokuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Simba Day akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wakati anatoka uwanjani hapo, Waziri huyo alikutana na malalamiko ya waandishi wa habari za michezo wakilalamika kitendo cha Mwandishi mwenzao kupigwa na Polisi akiwa katika kazi.

Baada ya jitihada za waandishi kutaka Polisi wamuachie Mwandishi mwenzao kushindikana walisogea sehemu ya kutokea VIP uwanjani hapo na kukutana na Waziri Lugola akiwa anaelekea kweye gari lake ndipo walipo msimamisha na kutoa malalamiko yao.

"Kila mmoja nyie waandishi na jeshi la Polisi mpo hapa kufanya kazi zenu..., niwaombe TFF na bahati nzuri Rais wake yupo hapa, waweke utaratibu mzuri wa waandishi kufanya kazi zao ili wasisuguane na Polisi," alisema Lugola.

"TFF inapaswa kuonyesha geti litakalotumiwa na waandishi na kuwaeleza Polisi hili waandishi wasibugudhiwe, niwaahidi tukio kama hili halitotokea tena, tutakaa na Polisi kuwaeleza lakini pia TFF watalifanyia kazi," alisema Lugola.

Baada kauli hiyo, Lugola aliamuru Mwandishi aliyepigwa na kushikiliwa na Polisi kuachiwa na kutolewa kwenye gari (Kalandinga).

Matukio ya mvutano wa Polisi na waandishi wa habari kwenye viwanja hasa panapofanyika mechi kubwa yamekuwa yakijitokeza Mara kwa Mara.

No comments:

Post a Comment