Tuesday, February 20, 2018

TAKUKURU YAPOKEA TAARIFA 204 ZA VITENDO VYA RUSHWA TANGA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Tanga (Takukuru) imepokea taarifa 204 za vitendo vya rushwa kutoka kwa wananchi wakizilalamikia idara mbalimbali za serikali na sekta binafsi.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga,Christopher Mariba wakati akitoa taarifa za utendaji wao kwa waandishi wa habari kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba mwaka 2017.Alisema taarifa hizo ni ongezeko la taarifa 30 sawa na asilimia 17 ukilinganisha na kipindi cha miezi sita iliyopita ambapo taarifa zilizo pokelewa ni 174.

Aidha alisema katika taarifa hizo 52 zilihusu serikali za mitaa, ardhi/ mabaraza ya ardhi 33,vyama vya siasa 28,Polisi 23,Elimu 18,Mahakama 16,Afya 15,Kilimo 8,Tasaf 5,Bandari (TPA) 1,Maji 1,Ushirika 1,Uhamiaji 1,Tanesco 1 na Misitu 1.

Mkuu huyo alisema kati ya taarifa hizo 204 zilizopokelewa taarifa 92 zinaendelea kuchunguzwa wakati nyengine 66 uchunguzi wake ulikamilika na majalada kufungwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi.Aliongeza kuwa taarifa 46 zilihamishwa kwenye idara nyengine kwa sababu zilikuwa zikihusiana na makosa chini ya kuzuia na kupambana na rushwa.

No comments:

Post a Comment