hama cha taifa cha wamiliki wa bunduki Marekani (NRA) kimeonekana kubadilisha msimamo wake na kuunga mkono udhibiti wa vifaa ambavyo hutumiwa kuimarisha uwezo wa bunduki.
Kifaa kama hicho kilitumiwa na mwanamume aliyewaua watu 50 kwenye tamasha mjini Las Vegas.
Kundi hilo limesema: "Vifaa hivyo ambavyo huwezesha bunduki ambazo zina uwezo fulani wa kufyatua risasi mfululizo kuwa bunduki kamili za kufyatua risasi mfululizo kwa kujiendesha yenyewe."
Chama cha Republican kimesema kwamba kitajadili uwezekano wa kupiga marufuku kifaa hicho kwa jina 'bump-stock' ambacho huondoa haja ya mtu anayetumia bunduki isiyo na uwezo kamili wa kufyatua risasi mfululizo kutumia bega lake kuidhibiti bunduki wakati wa kufyatua risasi.
Wabunge wanapanga kuandaa vikao na kujadili mswada wa kupiga marufuku kifaa hicho.
Alhamisi, NRA walitoa wito kwa wadhibiti wa bunduki "kuchunguza mara moja iwapo vifaa hivyo vinafuata sheria za serikali ya taifa."
Rais Donald Trump baadaye aliwaambia wanahabari kwamba utawala wale utafikiria uwezekano wa kuzipiga marufuku "muda mfupi ujao."
"Baada ya shambulio hilo la kinyama Las Vegas, Wamarekani wanatafuta majibu kuhusu jinsi ya kuzuia maafa kama haya siku za usoni," wakuu wa NRA Wayne LaPierre na Chris Cox waliandika kwenye taarifa.
Hata hivyo, wamewakosoa wanasiasa ambao wanatetea udhibiti zaidi wa bunduki, wakisema kwamba "kupiga marufuku raia wanaotii sheria kumiliki bunduki kwa sababu ya kitendo cha kihalifu cha mwendawazimu hakutazuia mashambulio kama haya siku za usoni.Taarifa hiyo ndiyo ya kwanza kutoka wka chama hicho tangu shambulio hilo la Jumapili Las Vegas ambapo watu 58 waliuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa.
NRA hata hivyo wamesema vifaa hivyo viliidhinishwa na Shirika la Kudhibiti Silaha, Pombe na Tumbaku wakati wa utawala wa Rais Obama.
Msemaji wa White House Sarah Sanders, akizungumza na wanahabari baada ya taarifa ya NRA kutolewa, amesema: "Wanachama wa vyama vyote viwili na mashirika mengi wote wanapanga kuangalia upya vifaa hivyo. Tunakaribisha hilo na tungependa kuwa sehemu ya mazungumzo yanayoendelea."
Kwenye taarifa yao, NRA walihimiza Bunge la Congress kupitisha pendekezo lao la kuhakikisha haki za kumiliki silaha zinatekelezwa kote nchini humo.
Chama hicho kinataka wamiliki wa silaha wenye leseni za kubeba silaha wakiwa wamezificha kwenye jimbo moja waruhusiwe kuingia kwenye majimbo mengine bila kujali iwapo sheria za umiliki wa silaha huko ni tofauti.
No comments:
Post a Comment