Monday, September 18, 2017

SERIKALI YATOA ANGALIZO KUEPUSHA VIFO MAENEO YALIYO KARIBU NA KAMBI ZA JESHI


Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Idd Kimanta amewataka wananchi wanaochunga mifugo eneo linalotumika kwa mafunzo ya kijeshi kutoa taarifa kwenye kambi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kuepusha vifo.

Kimanta alitoa kauli hiyo jana katika Kijiji cha Nafco, Kata ya Loksale wakati wa maziko ya watoto watatu waliopoteza maisha wakichunga mifugo ya familia kwenye eneo la mafunzo ya jeshi la Loksale wilayani hapa, Ijumaa iliyopita.

Watoto hao; Johnson Daniel Mollel ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Nafco, Emmanuel Saitabau Mollel wa darasa la kwanza na Samweli Nyangusi walipoteza maisha wakati wakichunga baada ya kulipuliwa na bomu.

Kimata alisema kwa muda mrefu kumekuwa na ushirikiano kati ya kambi za JWTZ zilizopo wilayani humo na vijiji vinavyozunguka maeneo ya mafunzo, hivyo tukio hilo ni la bahati mbaya.

Brigedia Jenerali Rajab Hunt kutoka Kambi ya Monduli alisema tukio hilo halikutarajiwa kwa kuwa Serikali inanunua silaha kwa ajili ya ulinzi na si kuwadhuru wananchi.

Mkuu wa Brigade ya Mbuni, Brigedia Jenerali Athanas Mbonye alisema wananchi wasiwe na wasiwasi kwa sababu jeshi lipo kuwalinda na watoe taarifa wanapoona vifaa wanavyovitilia shaka.

Kiongozi wa mila wa jamii hiyo ya wafugaji, Loibanguti Loondawa alisema tukio hilo limeleta majonzi kwa familia na ni la bahati mbaya kwa kuwa halikuwa limekusudiwa.

Oktoba, 2012 watoto watano wakiwamo watatu wa familia moja walikufa kwa kulipukiwa na bomu wilayani Karagwe mkoani Kagera walipokuwa wakilichezea baada ya kuliokota kwenye vyuma chakavu.

No comments:

Post a Comment