Tuesday, September 19, 2017

KILICHOFANYA UTETTEZI WA MANJI KUSOGEZWA HADI SEPTEMBA 25

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, 'imepiga kalenda' kusikiliza ushahidi wa utetezi wa kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili mfanyabiashara Yusufally Manji.


Kesi hiyo 'imepigwa kalenda' baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis kuwa na udhuru wa kikazi na Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayeisikiliza kuridhia ombi la Jamhuri.

Vitalis alidai jana kesi hiyo, ilipangwa kuendelea na ushahidi wa utetezi, lakini amepata udhuru wa kikazi na kuomba tarehe nyingine ya kuendelea.

Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa mfululizo kuanzia Jumatatu mpaka Jumatano ijayo.

Kabla ya kupangwa tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hiyo, hakimu alimuonya Manji kwa kuchelewa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

Manji alidai kuwa aliwasiliana na wakili wake kwasababu alikwenda hospitali na kwamba tukio hilo halitajirudia tena.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View, jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

No comments:

Post a Comment