Tuesday, August 29, 2017

WAFUNGWA MAGEREZA KUPATIWA KAZI KWA MIKATABA MAALUMU

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameliagiza jeshi la Magereza na idara zingine zenye mashirika ya uzalishaji ambazo zipo chini ya wizara yake zifanye uzalishaji mali pamoja na kuwatumia wafungwa katika kufanya kazi ndani ya jeshi.

Waziri Nchemba ameongea hayo akiwa katika ufunguzi wa nyumba tano za maaskari wa jeshi la magereza mkoa wa Arusha nyumba zilizojengwa kwa kutumia fedha za shirika la magereza la uzalishaji mkoani humo.

Mh. Nchemba ametoa rai kwa jeshi hilo kuona kama inawezekana jeshi hilo kutumia wafungwa ambao wamemaliza mafunzo yao na wakaona wamerekebika kitabia na kuwachukua waendelee kufanya kazi kwa mkataba katika mashirika hayo kwani itarahisisha kupunguza wahalifu zaidi kuliko kwenda uraiani wakiwa hawana uwezo wakufungua biashara na kurudia makosa.

Naye mkuu wa Magereza Tanzania Dr Juma Malewa amewataka wananchi na mashirika ya umma na serikali kutumia jeshi la Magereza nchini katika shughuli za ujenzi kwani gharama zake ni nafuu sana lakini zenye ubora zaidi.

Kwa upande wa Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoa wa Arusha, Hamis Nkabasi amesema nyumba hizo zimetumia gharama ndogo za ujenzi kwasababu rasilimali watu wametumia askari wenye ujuzi wa ujenzi na wafungwa ambapo imegharimu milioni 50 kila nyumba na itaweza kuchukua askari 12 ambapo zote zitachukua askari 60 na kama wangechukua kampuni kujenga basi ingegharimu fedha nyingi zaidi.

No comments:

Post a Comment