Kocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog.
KOCHA wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kuwa, wiki hii ya mwisho katika kambi yao ya Afrika Kusini, atakuwa akiwapa zaidi wachezaji wake mbinu za uwanjani kwa lengo la kutafuta muunganiko, lengo likiwa ni kuandaa mapema mbinu za ushindi baada ya kuwa ameshamaliza kazi ya mazoezi magumu.
Simba ambayo imeweka kambi nchini Afrika Kusini ya kujiandaa na msimu ujao, inatarajiwa kurejea nchini Jumapili ijayo kujiandaa na tamasha lao la Simba Day, litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu.
Kambi hiyo iliyoanza Julai 17, mwaka huu, hii ni wiki yao ya mwisho ambapo jana Jumanne walicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Orlando Pirates, huku kesho Alhamisi ikitarajiwa kucheza na Bidvest Wits.
Timu hizo zote zinashiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini. “Wiki ya mwisho ndiyo wiki ya kumaliza kila kitu kwenye maandalizi yetu haya, utakuwa ni muda muafaka kwangu kuwaunganisha vijana wangu kwa kuwapa mbinu za uwanjani zaidi baada ya muda mrefu kufanya mazoezi ya fiziki.
“Naamini baada ya hapo, walinzi watakuwa wameshaiva katika suala zima la kulinda lango, lakini pia hata washambuliaji wakipata mbinu za kufunga mabao na viungo wakifahamu kazi yao ipasavyo.
“Kwa jumla itawafanya wachezaji wote kuelewana na kuleta matokeo mazuri msimu ukianza.
“Nataka tukirudi tuwe tumeshakamilika kila idara na timu iwe tayari tu kwa kuanza msimu mpya, najua tutakuwa na muda mrefu kidogo umebaki kabla ya kuanza kwa ligi, lakini mazoezi ya huku Afrika Kusini hasa haya ya mwisho ndiyo ya kujijenga zaidi kiuchezaji baada ya kuwa tumeshamaliza kazi ngumu ya uwanjani, naamini tunaweza kupambana na timu yoyote sasa,” alisema Omog. Ukiachana na mchezo wa Simba Day, mechi nyingine ya Simba itakuwa ni ile ya Ngao ya Jamii kati ya timu hiyo na Yanga Agosti 23, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment