Thursday, August 10, 2017

MADIWANI LINDI WAIOMBA SERIKALI IWADHIBITI TEMBO

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Lindi, wameiomba serikali ichukue hatua za haraka kuwadhibiti tembo wanaoharibu mazao ya wakulima katika vijiji vilivyopo katika wilaya hiyo.

Wito huo kwa serikali umetolewa leo kwenye kikao cha madiwani  kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo uliopo katika manispaa ya Lindi.Walipokuwa wanawasilisha taarifa za shuguli za maendeleo zilizofanyika kwenye kata zao katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2016 /2017.

Madiwani hao walisema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazao kwenye mashamba ya wakulima unafanywa na tembo katika baadhi ya vijiji vilivyopo katika wilaya hiyo. Hali ambayo inaweza kusababisha upungufu wa chakula kwenye vijiji hivyo.

Diwani wa kata ya Manara, Halima Mwambe alisema tembo wameharibu  ekari 76 za mazao ya kilimo katika vijiji vya Ntene na Liganga. Hata hivyo hakuna juhudi zilizofanyika ili kuwadhibiti. Mwambe kwa masikitiko makubwa alisema tembo hao wasipo dhibitiwa kunauwezekano mkubwa wa kuharibu mashamba mengine.

Hivyo kusababisha upungufu wa  chakula. Wakati serikali imekuwa ikisisitiza haitapeleka msaada wa  chakula kwenye maeneo ambayo mazao ya kilimo yanasitawi na hakuna sababu za upungufu wa chakula katika maeneo hayo.
 "Tatizo hili ni kubwa, tembo kwa sasa ni janga. Hatua za haraka zisipo chukuliwa kata yangu inaweza kukumbwa na upungufu mkubwa wa chakula," alisisitiza Mwambe.

Maelezo ya Mwambe yaliungwa mkono na diwani wa Navanga, Rashid Mkuya, ambae alisema tatizo tembo wilayani humo linachukuliwa na kutazamwa kwa wepesi kuliko madhara yatayotokea hapo baadae. Akibainisha kuwa awali tembo waliharibu mazao katika vijiji vya kata za Kilolombwani na Mvuleni pekee . Hata hivyo hakuna hatua za maana zilizochukuliwa.

Alisema kutokana na kuzembea kuwadhibiti, tembo hao wamesambaa, kufika na kuharibu mazao kwenye kata nyingine. Ikiwamo Manara, Namupa, Kiwawa na Nyangao. Hivyo umefika wakati serikali iingilie kati kudhibiti uharibifu huo ambao madhara yake ni makubwa.

Nae diwani wa kata ya Mvuleni, Idarous Manzi, alianza kutoa wito kwa mkuu wa wilaya hiyo atangaze kuwa tatizo la tembo ni janga. Tembo hao wasingeharibu mazao kwenye mashamba yaliyopo kwenye vijiji na kata nyingine iwapo wangethibitiwa haraka walipoanza uharibifu kwenye kata za Mvuleni na Kilolombwani. "Wakati tunalalamika, wangine mlitucheka. Wengine masharifu sisi, leo wamefika Nyangao, Manara na Namupa. Wasipodhibitiwa watafika kwenye kata zote na ndipo wilaya itakapokabiliwa na janga la njaa," alichekesha na kutahadharisha Idarous.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Methew Makwinya (diwani wa kata ya Nyangao) alikiri kuwa tatizo hilo ni kubwa na nikweli kwamba baadhi ya mashamba kwenye kata yake yameharibiwa na tembo. "Kibaya zaidi sheria inazuia wasiuwawe, bali tuwasake au tutwange pilipili tukamwage kwenye mashamba. Sote tunajua kwamba mshahara wa kutwanga pilipili ni kukohoa ,"Makwinya alichekesha na kueleza ukubwa wa tatizo hilo.

Licha ya kusema hayo, mwenyekiti huyo aliwaondoa hofu madiwani hao nakuwambia mipango kabambe na ya haraka inafanyika ilikuwadhibiti tembo hao. Ikiwamo kuwasiliana na waziri mwenye dhamana ya maliasili na utalii zichukuliwe hatua za haraka za kuthibiti tatizo hilo.

Miaka michache iliyopita, ilielezwa kuwa kuwa idadi ya tembo ilikuwa inapungua kwa kasi kutokana na kuuwawa na majingili. Hali iliyosababisha serikali kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na ujangili. Huku jumuia za kimataifa zikizibana nchi ambazo ni masoko makubwa ya pembe za tembo ziache kufanya biashara hiyo.

Uhenda hali hiyo ni ushahidi wa matokeo chanya ya juhudi za serikali na jumuia za kimataifa za kudhibiti ujangili na biashara ya pembe za tembo (ndovu)

No comments:

Post a Comment