Tuesday, August 1, 2017

HOFU YA NJAA YAIKUMBA KIBAHA

Wakazi wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha wanaolima katika ukanda wa bonde la mto Ruvu  wako hatarini kukumbwa na janga la njaa, kutokana na mashamba yao kuharibiwa na wadudu waharibifu na mengine kuchukuliwa na mafuriko yaliyotokea kipindi cha masika mwaka huu.

Hayo yalibainika katika kikao cha madiwani kilichofanyika juzi, ambapo pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika baraza hilo  ilibainika mashamba yaliyoharibiwa ni hekari 1,042, ambapo kati ya hizo hekari 226 za mazao mbalimbali zimeshambuliwa na  wadudu na 816 zimechukuliwa na mafuriko.

Kata zilizoathiriwa na wadudu ni Dutumi, Kikongo, Kwala, Ruvu, Mlandizi , Mtongani na  Mtamba na mazao yaliyokuwa yakilimwa ni mahindi, mpunga, mtama na mboga. Mazao yaliyoshambuliwa zaidi ni mahindi na mpunga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Mazingira, Ramadhani Chezeni, alisema hatua walizochukua ni kuwashauri wakulima   wanunue dawa ili kunyunyizia kwenye mazao na wale ambao mashamba yao yaliharibiwa na mafuriko walishauriwa wanunue mbegu na kupanda upya mazao mengine hasa mahindi.

Hata hivyo, madiwani na wabunge walionyesha kutoridhishwa na majibu hayo na kumtaka mkurugenzi na wataalamu wake kuhakikisha wanawasaidia wananchi kwa njia nyingine badala ya kutoa ushauri tu.

“Hawa wananchi watakufa njaa, siungi mkono kutoa ushauri tu, halafu dawa wanunue wenyewe, mbegu wanunue wenyewe kama mtu hana uwezo atafanyaje?” alihoji Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mchafu na kuongeza:

“Lazima halmashauri mtenge bajeti ya maafa ili kuwasaidia wananchi wanapopata majanga kama haya.”

Ofisa kilimo wa wilaya, Zahoro Thabiti, alithibitisha kuwapo kwa wadudu waharibifu na kusema wameleta athari kubwa na kuwa hata dawa zilizokuwa zinashauriwa zinyunyiziwe kuua wadudu zimeshindwa kufanya kazi.

“Ni kweli athari ni kubwa, tumeshauri wanunue da
wa aina tatu, lakini zote hazikuweza kuua wadudu, tukashauri walime mbinu rafiki, lakini pia imeshindikana kwani wadudu hao wana tabia ya kujibadilisha kulingana na mazingira na wanajificha,” alisema Zahaoro.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,  Mansuri Kisebengo, alimtaka mkurugenzi wa halmashauri kukaa na wataalamu wake kutafuta mbinu mbadala ya kuwasaidia wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa wizarani ili wasaidiwe kitaalamu zaidi.

“Mkurugenzi na timu yako  mtupe majibu, tunafanya nini ili kuwanusuru wananchi wetu na janga la njaa, wamepata mafuriko hakuna msaada, wamepata athari katika mazao kimya, kikao kijacho tupate majibu ya kuridhisha, alisema Kisebengo.

Kisebengo alisema katika bajeti ya mwaka huu, Halmashauri kwa kuona hilo, imetenga Sh. milioni 32 zitakazowasaidia wananchi kwa ajili ya dharura mbalimbali ikiwamo majanga ya mafuriko na njaa.

No comments:

Post a Comment