Tuesday, July 11, 2017

TFF YAPELEKA VYETI VYA WAGOMBEA NECTA

Dar es Salaam. Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imepanga kutinga katika ofisi za Baraza la Mitihani nchini (Necta) kwa ajili ya kuhakiki vyeti vyote vya wagombea waliopitishwa katika usaili.

Hivi karibuni, kamati hiyo ilipitisha majina ya wagombe huku wengine wakikatwa kwa kukosa sifa ikiwemo kushindwa kuwasilisha vyeti vya elimu ya kidato cha nne kama kanuni na taratibu za uchaguzi zinavyowataka.

Miongoni mwa wagombea ambao waliishia hatua ya usaili ni kocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' na nyota wa zamani wa Taifa Stars, Bakari Malima ambao walidaiwa kutowasilisha vyeti vyao vya kidato cha nne.

 Hata hivyo Julio ameweka ngumu na kudai kuwa atakata rufaa kwani cheti chake kilipotea na alipeleka uthibitisho huku Malima yeye akikiri kupeleka cheti cha kuhitimu (leaving certificate) na kwamba hataka rufaa.

Julio alisema kuwa kamati hiyo ilipaswa kwenda kujiridhisha Necta ndipo watoa uamuzi wao wa kumkata kwani ana uhakika ana cheti cha kidato cha nne tofauti na kamati hiyo ilivyoamua.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli alisema; "Nadhani wengine mmesikia wakilalamika kuwa wamekatwa wakati wana vyeti vya kidato nne, sisi hatuhitaji 'leaving certificate'(cheti cha kuhitimu kinachotolewa shuleni kama asante kwa kushiriki) tunahitaji cheti cha matokeo kinachotolewa na Necta watu watambue hilo.

"Tutakwenda Necta na majina yote ya wagombea waliopita ili kuhakiki vyeti vyao, kama kuna mgombea amepita wakati cheti sio chake ama kwa njia anayoijua yeye basi ataondolewa kwenye mchakato huo, watakaopita ni wale ambao elimu zao zinatambuliwa na Baraza hilo," alisema Kuuli.

No comments:

Post a Comment