IGP, SIMION SIRRO.
MKAZI wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Olivia Robert anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mwanaye baada ya kumpa kipigo cha zaidi ya saa 10 usiku wa juzi, akimshutumu kumwibia sh. milioni 1.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu wengine wawili wanashikiliwa na Jeshi hilo pia.
Joshua Benjamin (14) ambaye alikuwa akisoma darasa la Saba katika Shule ya Msingi Ukonga, anadaiwa kupigwa usiku kucha na mama yake huyo ambaye baadaye alimfunga kwa kamba kwenye mti, nje ya nyumba yake, hadi saa 11 alfajiri alipogundulika kuwa ameshakufa.
Tukio hilo, mashuhuda walisema jana, lilisababisha taharuki kubwa mtaani hapo kwani baadhi ya wakazi walitaka kumpiga mama huyo kabla ya polisi kufika na kumuokoa.
Mmoja wa majirani wa mama huyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, aliiambia Nipashe kuwa walianza kusikia kelele za mtoto huyo akiomba msaada tagu usiku huku mama huyo akiendelea kumpiga.
"Tulisogea hadi jirani na dirishani kwake," alisema shuhuda huyo na "tukamkataza."
"Tulimwambia adhabu hiyo inatosha kwa mtoto maana hadi mtoto aliishiwa nguvu, (hakutusikiliza) tukaondoka na kumuacha akimpiga tu.
Mtoto huyo amefariki ikiwa ni miaka miwili tangu kifo cha baba yake, jirani huyo alisema zaidi.
"Mume wa huyu mama tumemzika mwaka juzi, tuliumia majirani tukawaza pengine baba yake angekuwepo angemsaidia kumuokoa kijana yule.
MTOTO MWINGINE
Jirani mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Subira alisema chanzo cha kipigo ni madai ya mama huyo kuibiwa Sh. milioni 1 na mwanawe huyo.
"Cha ajabu ni kwamba ana mtoto mwingine mkubwa, na mle ndani kuna ndugu zake wengine sasa kwa nini asiwafikirie hao?" Alisema Subira.
"Alimpiga vibaya mno, yaani alimpiga utafikiri anapiga kibaka.
"Watu wengi tumeshuhudiia akimpiga na yeye ameokolewa na polisi la sivyo watu wangemmaliza."
Shuhuda mmoja aliliambia gazeti hili kuwa mwanamke huyo ana watoto wanne akiwamo marehemu ambaye ni wa tatu kuzaliwa. Wa kwanza amemaliza kidato cha nne, wa pili kidato cha pili na wa nne anasoma shule ya awali.
Alisema pia kwenye familia hiyo kuna mtoto wa kufikia wa mama huyo, wa marehemu mume wake.
Imeelezwa kuwa mtoto huyo alifariki saa 4 asubuhi baada ya mwanamke huyo kuona mtoto wake haamki, aliamua kupiga simu kwa watu wake wa karibu kuomba msaada.
Kamanda Hamduni aliiambia Nipashe jana kuwa watu wawili akiwamo mwanamke huyo wanashikiliwa na polisi tangu juzi.
"Ni kweli tukio hilo limetokea huko Kinyerezi na tunawashikilia vijana wawili pamoja na mwanamke huyo kwa ajili ya upelelezi," alisema.
No comments:
Post a Comment