Matukio ya watu kuchukua maamuzi ya kujiua katika manispaa ya Shinyanga yanazidi kushika kasi ambapo jana Jumapili June 18,2017 majira ya saa 10 alfajiri kijana aitwaye Paulo Ezekiel (17) mkazi wa mtaa wa Mazinge kata ya Ndembezi alifariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba juu ya mti jirani na nyumba yao.
Inaelezwa kuwa huenda ni ugumu wa maisha ndiyo umechangia kifo cha kijana huyo kwani enzi za uhai wake alikuwa analalamika kuwa maisha ni magumu.
Baba mzazi wa marehemu Ezekiel Paulo anasema majira ya saa 10 alisikia mlango wa chumba cha kijana wake ukifunguliwa akadhani pengine ametoka kwenda kujisaidia lakini hakurudi tena ndipo alipoingiwa na wasiwasi na kuanza kumsaka.
“Tuliamshana tukaanza kumsaka kila mahali baadaye tukamuona akiwa juu ya mti jirani na nyumba yetu tayari amefariki dunia”, ameeleza Paulo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Jumanne Murilo amethibitisha kutokea kwa tukio.
Matukio ya watu kuchukua uamuzi wa kujiua yameanza kukithiri katika manispaa ya Shinyanga ambapo ndani ya mwezi mmoja huu wa Juni hili ni tukio la nne.
Tukio la kwanza ni la Luhende Lusangija (34) mkazi wa kata ya Ngokolo aliyejiua kwa kamba,la pili ni la Mwenyekiti wa waendesha bodaboda katika manispaa ya Shinyanga Jacob Paul mkazi wa kata ya Ngokolo aliyejiua kwa waya wa simu la tatu ni la Saada Elias mkazi wa kata ya Ndembezi aliyekatisha maisha yake kwa kujichinja kwa kisu na chupa ya soda.
No comments:
Post a Comment