Tuesday, June 20, 2017

BAJETI YA SERIKALI KUPITISHWA LEO


Ikiwa bajeti ya serikali inatarajiwa kupitishwa na wabunge mjini Dodoma leo, wabunge wamendelea kuunga mkono juhudi za Rais John Mgufuli kwa kulinda rasilimali za nchi huku wakisisitiza kuwa vita ya madini ni vita ambayo kila mtu bila kujali itikadi za kisiasa anaiunga mkono.

Akichangia mjadala wa Taarifa ya hali ya uchumi 2016 na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliyowasilishwa bungeni Juni 8 mwaka juu, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, alimpongeza Rais Dk Magufuli na kuwa ni wakati wa kumuunga mkono kutokana na kazi kubwa aliyofanya kwa kusimamia mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi ‘makinikia’ na kusisitiza haja ya kuunga mkono pia juhudi za marais waliopita.

“Rais ameonyesha mfano mzuri, na kwa mjadala unavyoenda watu wengi wanamuunga mkono wanaweza kupatikana wachache ambao pengine wana mawazo tofauti, lakini hiyo haitufanyi tusisonge mbele na msimamo wa kulinda rasilimali za nchi yetu,” alisema. Alisema juhudi za kuzilinda rasilimali za nchi, hazijaanza kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, bali zilianza tangu utawala wa serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere.

Nape alisema wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, kuna mambo aliyafanya katika kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa na kwamba kuna mambo alifanya hata kama kuna mapungufu. Awamu zingine ni Awamu ya Pili ya Ali Hassani Mwinyi, ya tatu, Benjamin Mkapa na wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. “Hakuna haja ya kupuuza juhudi za watangulizi wake kwa sababu nao walitoa mchango hata kama itaonekana kulikuwa na mapungufu, lakini kwa nafasi zao walitimiza wajibu.

Tunatakiwa tutambue na kuheshimu michango yao badala ya kubaki tunawanyooshea vidole kama vile hawakufanya lolote,” alisema na kusisitiza kuwa Rais Magufuli ameifikisha nchi katika hatua kubwa zaidi. Aliongeza kuwa, “Kelele zisiturudishe nyuma lazima tusonge mbele kwa sababu vita hii ni takatifu, lakini tusipuuze katika kelele nyingi kwani kunaweza kukawa na ushauri mzuri ndani yake.

Hii vita ni ya kwetu wote, sasa tusitoboane macho tusitupiane vijembe visivyokuwa na sababu, ni wakati wa kuileta nchi yetu pamoja twende tukapigane vita tuishinde.” Kuhusu uchumi wa gesi na mafuta, Nape alirejea upotoshwaji wa taarifa na kuwa zilijaa chumvi nyingi badala ya ukweli kwamba faida ya gesi ingeweza kuonekana baada ya miaka 20 au 30, jambo ambalo lilisababisha vurugu. Alitumia fursa hiyo kuihoji serikali utekelezaji wa mradi wa mitambo ya kuchakata gesi, ambao alisema kukamilika kungeleta manufaa ya haraka kwa wananchi wa eneo hilo.

Heche aunganishwe Mbunge wa Viti Maalum, Jacline Msongozi (CCM), alilitaka Jeshi la Polisi kumkamata Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) na kumuunganisha kwenye kesi ya watu waliovamia mgodi akiwa mtuhumiwa namba moja, kwa sababu ndiye aliyehamasisha uvamizi huo. Alisema Rais Magufuli hajahamasisha wananchi kuvamia migodi, hivyo waliovamia mgodi wa North Mara ni wahalifu kama wahalifu wengine.

Kauli hiyo ilimnyanyua Heche ambaye awali aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Heche alisema “Kama mlivyosoma kwenye vyombo habari, jana na leo asubuhi wananchi wa Tarime eneo la Nyamongo, wamemuunga Rais mkono kwa vitendo, kwa kuingia kwenye mgodi wa North Mara kuzuia wizi ambao kamati zote za rais zimethibitisha na rais amewatangazia wananchi.

“Sasa mwenyekiti jambo la ajabu ni kwamba polisi wanatumia nguvu kubwa sana kupiga wananchi kuwaumiza, kinyume cha utaratibu wa rais alivyoagiza. Sasa mwenyekiti naomba mwongozo wako,” Akipinga hoja ya kuunganishwa, Heche alimtaka mbunge kufuta kauli yake na kuwa kama anataka aunganishwe kwenye kesi hiyo, basi mbunge aliyetoa hoja afanye hivyo.

Hata hivyo, Jacline alisema hakuna sehemu yoyote ambayo Rais Magufuli ameagiza wananchi wavamie migodi na kwamba wanaofanya hivyo, ni wahalifu kama wahalifu wengine, hivyo alilitaka jeshi la polisi kuwachukulia hatua kali. Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) alisema Rais Magufuli ameonyesha jambo jema kwa kuunda tume mbili zilizofanya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu.

Nkamia aliwataka wapinzani na wanaCCM, kuungana kwa pamoja kumuunga mkono rais kwa juhudi zake za kizalendo katika kuzilinda rasiliamli za taifa, “hakuna mwanaCCM mwenye kadi ya kijani zaidi ya mwenzie, hivyo tunatakiwa tusitengane katika hili.” Mohamed Mchengerwa, alisema nchi imefika hapa kutokana na kuwa na mikataba mibovu na kwamba mingi haifai, ambapo aliishauri serikali kuifanyia marekebisho sera ya madini.

Naye Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) aliishauri serikali kuwa makini kwenye sekta ya gesi ili isije ikaingia kwenye matatizo na kuiomba serikali kugawanya wilaya hiyo ili huduma za wananchi ziwe rahisi kuwafikia. Alisema Rais Magufuli amefanya kazi iliyotukuka kwa kipindi cha miezi 18 tangu alipoingia madarakani na utawala wake umeonesha dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi. Mbunge wa Tumbe, Rashid Alli Abdallah (CUF), alisema kuwataja mawaziri waliopita kwenye suala la makinikia sio sawa, na alishauri sheria zote za madini na maliasili zifumuliwe
.

No comments:

Post a Comment