Friday, May 26, 2017

TETEMEKO LA DUMU SEKUNDE 10 LILIVYOUAWA NA KUJERUHI MWANZA

 

KAMANDA WA POLISI, AHMED MSANGI.
Askari polisi mmoja alifariki dunia na mwingine mmoja, mtuhumiwa mmoja kupoteza fahamu jana kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga kwa sekude 10 katika maeneo machache ya mkoa wa Mwanza. Tetemeko hilo lililotokea jana saa 6:55 mchana.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alimtaja marehemu kuwa ni askari wa kike mwenye namba WP 4674, koplo Joyce Mwalingo.
Kamanda Msangi alisema WP Joyce alifariki akiwa katika eneo lake la kazi, akifanya mahojiano na mtuhumiwa katika kituo cha Polisi Misungwi kilichopo wilaya ya Misungwi mkoani hapa.
“WP Joyce alifariki dunia baada ya tetemeko lililotokea majira ya saa 6:55 mchana, wakati akifanya mahojiano huku akiwa na askari mwenziye WP 11954, Stela ambaye alipata mshtuko baada ya kupata taarifa ya kifo cha mwenzake," alisema Kamanda Msangi.
Alisema WP Stela alipelekwa hospitalini kwa matibabu kutokana na hali yake kuwa mbaya pamoja na mahabusu Mathias Saimon ambaye alizimia kwa mshtuko wa janga hilo.
Kamanda huyo hakuweza kutaja kipimo cha tetemeko hilo, lakini halikuwa na ukubwa wa janga la Septemba 10, mwaka jana lililokumba mkoa wa Kagera lililokuwa na nguvu ya 5.7 katika vipimo vya Richter, na kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa earthquaketrack.com ndilo kubwa zaidi katika historia kutokea nchini.
Tetemeko hilo lilisababisha vifo vya watu 18, majeruhi 190 na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.
Aidha, Kamanda Msangi alisema tetemeko hilo lilitikisa maeneo kadhaa ya wilaya za Kwimba, Misungwi na Nyamagana na kuzua hofu kwa watu kutokujua nini wafanye.
Alitaka wananchi, hususani waliojenga katika maeneo ya milimani, pembezoni mwa mawe, kuchukua tahadhari ya kutoka nje mapema pindi waonapo hali ya tofauti.
Meneja wa kampuni ya bima ya Jubilee Insurance, Jared Awando ambaye ni shuhuda wa tetemeko hilo alisema jengo ambalo ofisi yake ipo lilitikisika, hivyo yeye na wafanyakazi wote walitoka nje kwa kukimbia na kuungana na wananchi wengine ambao walionekana kuhangaika bila kujua cha kufanya.
Jackline Timo na Bahati John walisema wao walikuwa ndani ya nyumba wakifanya shughuli zao na pindi wakaona jengo linatetemeka ndipo wakachukua maamuzi ya kutoka nje haraka.
Tetemeko hutokeaje?
Mtaalamu wa masuala ya miamba, George John anasema ardhi ya dunia imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni tabaka la juu, la kati na la chini.
Anasema katika tabaka la kati mara nyingi kunatokea msuguano ama msukumo wa volcano ambao kila upande unavuta upande wake.
Anasema wakati kitendo hicho kinatokea ndipo mgongano unagonga katika tabaka la juu la uso wa dunia na kutokea tetemeko la ardhi.
“Ni mvutano ambao hautabiriki utatokea lini, hata utabiri wa hali ya hewa hawajui, ni kitendo ambacho hutokea chini ya ardhi ya dunia,” alisema John.
John anasema hata ziwa Victoria na Tanganyika yote yametokea kutokana na mvutano huo miaka bilioni 3.5 iliyopita.
Anasema maeneo kama Manyara, Kagera, Mwanza na Mara yapo katika bonde la ufa, hata nchi za Kenya, Rwanda na Uganda.
Anasema tetemeko lililotokea katika mikoa ya Mwanza na Kagera lilisababishwa na msuguano wa volkano, lakini ni tofauti na tetemeko lililotokea nchini Japan hivi karibuni ambalo lilisababishwa na msuguano wa miamba.

No comments:

Post a Comment