Wednesday, May 17, 2017

SIMBA, YANGA YAPIGANIA DILI LA MILIONI 100

Klabu ya soka ya Simba na Yanga zinataraji kutwa Sh Milioni 100 zitokanazo na Bonasi  kwa mshindi wa ligi kuu ya Vodacom (VPL) ambayo itakuwa ni  sehemu ya mkataba wa kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa na Yanga ambao wameingia leo.

Mkataba huo utakuwa ni wa miaka mitano na utagharimu kitita cha Sh bilioni 5.173 huku mwaka wa kwanza Yanga ikiingiza Sh milioni 950.

Katika mkataba walioingia na Simba, pia bonus ni Sh milioni 100 kwa atakayefanikiwa kuwa bingwa.

Mmoja wa Wakurugenzi wa SportPesa , Abbas Tarimba amesema leo kuwa mkataba wa Yanga na ule wa Simba haina tofauti na bingwa msimu ujao atalipwa Sh milioni 100 kutoka SportPesa.

"Kwa yule atakayefanikiwa kuchukua ubingwa wa Afrika, yeye tutatoa Sh milioni 250, hii ni sehemu ya bonus kwenye mkataba," alisema.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwashukuru SportPesa kuungana nao.

"Tunaamini ni sehemu ya kuleta mabadiliko, wamekuja kuunga nasi, tumewapokea na tunawaahidi ushirikiano. Hii ni kati ya kampuni nimeona kwa mara ya kwanza tumejadili mambo mengi. Mengine yatatokea huko mbele lakini ni mambo ya maendeleo," alisema.

Mkataba huo umesainiwa leo katika makao makuu ya klabu ya Yanga mbele ya waandishi wa habari.

Yanga inakuwa klabu ya pili kusaini mkataba na SportPesa baada ya Simba.

No comments:

Post a Comment