Monday, May 8, 2017

MTOTO WA SHULE ALIYEFARIKI ARUSHA ALINUSURIKA BOMU 2013


MTOTO aliyejeruhiwa kwa bomu lililorushwa katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti miaka minne iliyopita, Arnold Alex amefariki dunia kwa ajali ya basi la Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent juzi.
Arnold ambaye wazazi wake wanatoka Jumuiya ya Familia Takatifu katika Parokia ya Utatu Mtakatifu ya kwa Mrombo, ni miongoni mwa wanafunzi 33, walimu wawili na dereva waliofariki katika ajali hiyo.
Aidha, Arnold ni miongoni mwa watoto wanne wa shule hiyo waliofariki katika ajali hiyo, ambao wanatoka wote pia Parokia ya Utatu Mtakatifu hiyo.
Wengine ni Praise Mwaliambi, Hagai Lucas, Gema Gerald na mwingine ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Malera wilayani Karatu, majira ya saa tatu asubuhi wakati mvua ikinyesha, baada ya gari kushindwa kufunga breki, kuserereka na kutumbukia kwenye korongo.
Wanafunzi waliofariki dunia walikuwa kwenye gari aina ya Toyota Coaster lenye namba za usajili T871 BYS, mali ya shule hiyo.
Taarifa zilizoandikwa kwenye kundi la mtandao wa kijamii wa WhatsApp la Shirika la Neno la Mungu, ambazo zilikuwa zikiarifu taarifa ya kifo cha Arnold na wenzake katika parokia hiyo, ilisema alinusurika katika bomu lililorushwa kanisani Mei 5, 2013 lililoua watu watatu na kujeruhi wengine 50.
Kupitia kundi hilo, Paroko wa Parokia ya Utatu Mtakatifu, Castelino Peddey ambaye wakati wa mlipuko wa bomu kanisani alikuwa paroko huko, alisema Arnold ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika tukio lile la bomu.
“Kwa masikitiko makubwa tumepoteza vijana wetu, watoto wetu ambao pia ni wahudumu kanisani (alter boys). Tuwaombee wapate pumziko la milele,”
alisema Peddey huku akiwataja kwa majina na kuongeza, "Arnold miaka minne iliyopita alinusurika katika mlipuko wa bomu lililorushwa kanisani Olasiti."
Hivi karibuni, Arnold aliondolewa mwili chuma kilichowekwa mguuni mwake kama sehemu ya tiba, baada ya kujeruhiwa katika tafrani ya bomu lililorushwa kanisani na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lilitokea wakati waumini walipoanza misa ya uzinduzi wa kanisa hilo iliyoongozwa na aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Montecillo akisaidiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Kuu la Arusha, Josephat Lebulu.
Watu watatu waliuawa katika tukio hilo lililowaacha karibu watu 50 wakiwa majeruhi huku baadhi yao wakiwa wameumizwa vibaya.
Polisi ilimshikilia dereva mmoja pikipiki aliyetajwa kuwa Victor Ambrose kulisaidia jeshi hilo katika uchunguzi wake.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 20 wakati huo, alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kamuzora Mei 13, 2013, akisomewa mashtaka 21 ya kuua na kujaribu kuua.
Mtuhumiwa huyo, hata hivyo, hakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo kwa kuwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili yalipaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.
MWANAE PRAISEKatika hatua nyingine, Roland Mwaliambi anayeishi Dar es Salaam alisema kwa mara ya kwanza alipata taarifa ya ajali hiyo kupitia WhatsaApp kabla ya watoto wake waliopo jijini hapa kumpigia simu.
Alisema baada ya taarifa hiyo alilazimika kuchukua usafiri wa haraka wa ndege kuwahi Arusha ambako alithibitisha kwamba mwanae Praise ni miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo.
Alisema mwanae ambaye alionyesha kuwa na wito wa upadre alitarajia kujiunga na Seminari ya Maua iliyopo Moshi Januari mwakani na taratibu zilikwishafanyika za kujaza fomu ya maendeleo yake kitaaluma, lakini ndoto yake imezimwa ghafla.

No comments:

Post a Comment