Thursday, May 4, 2017

MTIKISIKO WA UCHUMI:BENKI 3 HATARINI KUFUNGWA

Hali ya mtikisiko wa uchumi uliozikumba taasisi nyingi, hasa za fedha sasa unazinyemelea benki tatu ambazo zinaweza kuwekwa chini ya uangalizi maalumu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama ilivyokuwa kwa Twiga Bancorp.

Twiga Bancorp, ambayo kwa sehemu kubwa inamilikiwa na Serikali, imewekwa chini ya uangalizi wa BoT baada ya madeni yasiyolipwa (NPL) kuzidi kiwango kinachotakiwa kisheria.

Hali hiyo inazinyemelea taasisi nyingine tatu za fedh; Benki ya Wanawake (TWB), ambayo pia inamilikiwa na Serikali, Ecobank Tanzania na Efatha Bank, ambayo inahusishwa na taasisi ya kidini ya Efatha, kwa mujibu wa uchambuzi wa The Citizen

Benki hizo tatu zimelimbikiza kiwango cha NPL kinachozidi asilimia 50 ya jumla ya mikopo iliyotolewa, huku kiwango cha Efatha kikifikia asilimia 63.

Wataalamu wa benki wanaamini kuwa kiwango cha NPL kinachozidi asilimia 15 ya jumla ya mikopo yote ya beki za biashara, kinaashiria uwezekano wa kuanguka.

Katika toleo la tisa la Hali ya Kiuchumi Tanzania, Benki ya Dunia ilitahadharisha kuhusu kukua kupita kiasi kwa kiwango cha NPL, ambacho kilifikia asilimia 9.5 mwaka 2016 kutoka asilimia 6.4 mwaka 2015.

Ripoti hiyo iliitaja TIB Development Bank ambayo kiwango chake cha NPL kilikuwa asilimia 38 katika robo ya kwanza ya mwaka 2017.

Hata hivyo, taarifa za fedha za benki za biashara za robo ya kwanza mwaka 2017 zinaonyesha hali ni mbaya zaidi kwa Efatha, TWB na Ecobank Tanzania.

No comments:

Post a Comment