Tuesday, May 23, 2017

JE WAFAHAMU MADHARA YA MAFUTA YA TAA?


Dar es Salaam. Siku chache baada ya gazeti hili kuandika habari za wanafunzi wa shule za bweni kuwekewa mafuta ya taa katika chakula ili kupunguza hamu ya ngono, Mkemia Mkuu wa Serikali Profesa Samweli Mnyele ameelezea madhara yanayoweza kumpata mtu aliyekula au kunywa mafuta ya taa.
Profesa Manyele ametoa ushauri wa kuepuka matumizi yake.
Katika uchunguzi wa Mwananchi ilibainika kuwa baadhi ya shule huweka mafuta ya taa kwenye chakula ili kupunguza mihemko kwa wanafunzi wa shule za bweni.
Akizungumza na gazeti hili jana Profesa Mnyele amesema kuna athari kadhaa zinazoweza kumpata mtu kutokana na kunywa mafuta ya taa lakini hilo hutegemea na namna yalivyoingia kwenye mwili. Amefafanua kuwa hadi sasa utafiti uliofanywa kuhusu mafuta ya taa ni kwa panya, ambaye amekuwa akitumiwa kwenye utafiti mwingi wa kisayansi.
Hata hivyo amesema; “Binafsi haiingii akilini kuhusu wanafunzi kulishwa chakula chenye mafuta ya taa kwa makusudi fulani, naamini kwamba ni hali hiyo inawezekana inachangiwa na kukosekana kwa elimu ya utunzaji wa chakula hasa kinapokuwa stoo.”
Profesa Mnyele amesema ingawa hakuna utafiti wa kisayansi ambao unaeleza jinsi mafuta ya yanavyopokelewa mwilini na yanavyoyeyuka, lakini kutokana na wingi wa kemikali kwenye mafuta hayo ni wazi kwamba yana sumu.
“Kwa kawaida mwili ukipokea sumu yoyote husambaa kwa kuingia kwenye mfumo wa damu, hupita kwenye mishipa ya moyo, maini na figo kwa ajili ya kuondolewa mwilini, lakini hakuna utafiti unaonyesha mafuta ya taa yanavyoondolewa mwilini,” amesema Profesa Mnyele.

No comments:

Post a Comment