Wednesday, April 5, 2017

SERENGETI BOYS WAPEWA MBINU MPYA ZA USHINDI NA MAKAMU WA RAIS



April 4, 2017, makamu wa Rais wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan aliipa mwaliko timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwa jili ya kupata nao chakula cha usiku ‘dinner’ pamoja na kuwaaga kabla hawajasafiri kuelekea Morocco kuweka kambi ya maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda Gabon kwenye michuano ya AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17.

Katika salam zake kwa Serengeti Boys, mama Samia alisema, vijana hao wajitahidi kupata ushindi ndani ya dakika 90 lakini kama itatokea maajabu kama yaliyotokea kwenye mechi yao ya kirafiki dhidi ya Ghana basi iwe ni sehemu ya mchezo lakini isiwe kawaida yao kutafuta ushindi wa kulazimisha dakika za lala salama.

“Matokeo ya mechi dhidi ya Ghana yalikuwa mazuri sana lakini mimi yalinipa hofu kidogo, kwa sababu kilichotokea ilikuwa ni miujiza. Ndani ya dakika 10 ulirudisha magoli mawili, sio kitu rahisi, kwa kawaida maajabu huwa yahana kanuni, kwa hiyo naomba msicheze kwa maajabu, chezeni ndani ya dakika 90,” alisema mama Samia wakati akizungumza na vijana wa Serengeti Boys nyumbani kwake.

“Kilichotokea kwenye mechi dhidi ya Ghana tukiwauliza mlitumia formula gani hamtoweza kunieleza ni uwezo wa Mungu kutaka yale yatokee, sasa naomba msicheze hivyo, chezeni ndani ya dakika 90. Hakikisheni dakika 90 zinakwisha mkiwa na ushindi wenu mkononi ikitokea maajabu kama yale basi iwe imetokea tu lakini msiseme kwamba watachoka tutawafunga wakati huu.”

“Ingekuwa waghana hawakufanya upuuzi wa kujiangusha mkapata dakika nyingi za nyongeza tungekuwa tumekwisha, lakini upuuzi wao wa kujiangusha ndio ukazaa dakika 10 mkaweza kupata sare, lakini sio mchezo mzuri.”

Makamu wa rais pia akatoa wito kwa viongozi pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo kuishi na kuwalea vijana hao kama marafiki zao lakini kuwarekebisha pale wanapokosea.

“Ushindi wa timu unategemea na viongozi mnawababaje watoto, mnawapa huduma gani, mnazunguza nao vipi. Pamoja na kwamba ni watoto lakini wanataka kubebwa kama marafiki pia kwamba kama wanakosea warekebishwe lakini kama marafiki, wanapozidi utukutu chapa kwa sababu wanasema huruma hailei mwana.”

“Mpaka hapa tulipofika ili hawa waweze kufanya vizuri wanahitaji matunzo mema , hamasa, upendo wenyewe wanahitaji mshikamano na kupendana wao kwa wao kupendwa na walimu wao na viongozi wao hivyo ndivyo wanaweza kufanya vizuri. Kwa hiyo kwa upande wa viongozitunawakabidhi hii timu mnakwenda nayo nje ya nchi mtakaa nao kwa muda mrefu, hatupendi kusikia hili wala lile limetokea kwa hawa vijana.”

No comments:

Post a Comment