MBUNGE WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR ATAKA ZANZIBAR ILIPIWE DENI LA UMEME NA TANZANIA BARA
Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Jaku Hashimu Ayoub
ametaka makusanyo ya kodi na tozo mbalimbali za Serikali yapelekwe
Zanzibar ili kulipia deni la umeme.
Jaku alisema hayo wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, ambapo
alisema kuna kodi zinazolipwa Tanzania Bara, lakini hazipelekwi
Zanzibar kwa ajili ya kusaidia maendeleo ikiwamo kulipia deni hilo.
Mbunge aliyedai kuwa na ushahidi juu ya kauli yake hiyo na kwamba yupo
tayari kuutoa, alisema fedha hizo ni muhimu zikapelekwa ili zisaidie
ulipaji wa malimbikizo ya deni la umeme.
Machi 9, mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilitangaza
kuikatiaumeme Zanzibar kutokana na limbikizo la deni la zaidi ya
Sh275.38 bilioni.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema wameipa
siku 14 kuhakikisha kuwa inalipa deni hilo. Hata hivyo, siku chache
baadaye Tanesco ilitangaza kulipwa Sh10 bilioni kama malipo ya awali ili
isikate umeme visiwani humo.
Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Magomeni (CCM), Jamal Kassim
Ali alitaka kujua iwapo Serikali haioni haja ya kodi ya mishahara (paye)
kwa wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) isikusanywe
visiwani humo kwa ajili ya kusukuma maendeleo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji alisema kwa mujibu
wa Sheria ya Mapato sura ya 66, kifungu cha 4(a) na (b), kodi za kampuni
ni za Muungano na zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia, alisema hata kampuni ambazo zimesajiliwa Tanzania Bara lakini zinafanya kazi Zanzibar, kodi zake zinakusanywa Bara.
Naibu waziri alisema iwapo kampuni itakuwa imesajiliwa Zanzibar na ikawa
na matawi Tanzania Bara inatakiwa kulipa kodi yake Zanzibar.
No comments:
Post a Comment