Wednesday, April 12, 2017

Makamu wa Rais aushangaa mkoa wa Iringa

MAKAMU wa Rais,  Samia Suluhu Hassan,  amesema ni aibu kwa Mkoa wa Iringa unaoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula, kuwa miongoni mwa mikoa yenye utapiamlo

Akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa  wa Iringa baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mkoa anakofanya ziara ya kikazi, Samia alisema hali hiyo inatakiwa kuondoshwa kwa sababu haiendani na mazingira ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa Samia, Mkoa wa Iringa hautakiwi kuwa na utapiamlo kwa sababu unasifika kwa kilimo, ukusanyasaji wa mapato pamoja na kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba.

“Iringa ni kati ya mikoa 10 bora inayozalisha chakula cha kutosha ila mkoa huo unatia aibu katika eneo la utapiamlo na Ukimwi.

“Pamoja na hayo, nawapongezeni sana viongozi  wote wa Mkoa wa Iringa kwa sababu mnafanya kazi nzuri ya kutekeleza maagizo mbalimbali ya kitaifa yanayotolewa na Rais wetu, Dk. John Magufuli.

“Kweli mpo juu sana nami nawapongeza ila  siwezi kuwasifia kwa aibu hii ya watoto kuwa na udumavu kwa kukosa  lishe  bora na  hili la Ukimwi,” alisema Samia.

Pamoja na hayo, alisema ziara yake mkoani Iringa ni kunusuru Mto Ruaha Mkuu usitoweke na kwamba anakusudia kuwa na ziara nyingine mkoani Iringa azunguke mkoa mzima na  kutazama sekta moja baada ya nyingine.

Kuhusu fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), zinazotolewa na Serikali kwa familia zisizo na  uwezo, Makamu wa Rais aliwataka viongozi wa mkoa huo kusimamia utoaji wa fedha hizo kwaumakini wa hali ya juu.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza,alisema lishe kwa watoto walio chini ya  miaka mitano mkoani Iringa siyo nzuri na kwamba zinahitajika nguvu za ziada kutokomezahali hiyo.

No comments:

Post a Comment