Tuesday, April 25, 2017

MADIWANI CHADEMA WAPONZWA NA MAGUFULI



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewalima barua baadhi ya madiwani wake wa Halmashauri ya Jiji ya Arusha baada ya kujitokeza hadharani kuisifu Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, ingawa wenyewe wamesisitiza si unafiki kusifu maendeleo yaliyofanywa na serikali hiyo.

Wiki moja iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro alifanya ziara katika kata zote 25 za Jiji la Arusha ya kuangalia shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutatua kero za wananchi wa kata hizo.

Mbali ya mkuu wa wilaya kuwepo katika ziara hiyo, pia alikuwepo Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia na wakuu wote wa idara za jiji hilo, watendaji wa kata zote ikiwa ni kutaka kutatua kero za hapo kwa hapo zitakazoulizwa na wananchi wa kata husika na kupatiwa majibu.

Madiwani wa Chadema walioandikiwa barua na kutakiwa kujieleza kabla ya kesho Aprili 26, mwaka huu ni Diwani wa Kata ya Kimandolu, Elishadai Ngowi na Diwani wa Kata ya Terrat, Obeid Meng’oriki.

Nakala ya barua hiyo iliyoandikwa na Katibu wa Chadema Wilaya ya Arusha, Stephen Urassa, imewataka madiwani hao kujieleza ni kwa nini wameisifu Serikali ya Rais Magufuli katika mikutano ya hadhara ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha alipokuwa akifanya ziara katika jiji hilo. Urassa katika barua hiyo, alidai kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za Chadema, hivyo ni kwa nini madiwani hao wasichukuliwe hatua kwa uamuzi huo waliofanya unaodaiwa ni kinyume cha Katiba na kanuni za chama.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Diwani wa Kimandolu, Ngowi alikiri kupata barua hiyo na kusema atatimiza kile alichotakiwa kueleza katika barua hiyo. Diwani Ngowi alisema hakuwa mnafiki kumsifu Rais Magufuli hadharani katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa wilaya alipotembelea kata hiyo kwa kuwa anasifu kitu kilichofanywa katika kata hiyo na nchi kwa ujumla.

Alisema anaamini kuwa Serikali ya Jiji la Arusha pamoja na uongozi wa wilaya hiyo wakiongozwa na Kiranja Mkuu, Dk Magufuli wanafanya vema katika kuboresha miundombinu ya Jiji la Arusha na kutatua kero za wananchi, hivyo haoni kama ina tatizo lakini kuna baadhi ya watu ndani ya chama hicho wanapotosha ukweli. Diwani wa Kata ya Terrat, Meng’oriki hakupatikana kwa njia ya simu kueleza kama amekubaliana na hatua ya uongozi wa Chadema Wilaya ya Arusha kumwandikia barua hiyo kwa kosa la kuisifu serikali, kwani simu yake iliita bila ya kupokelewa.

Hata hivyo, baadhi ya madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani walijitokeza waziwazi kumsifu DED Kihamia kwa kazi nzuri anayofanya ya kujenga miundombinu ya jiji hilo na kuwa lenye hadhi kubwa kiasi cha kufananishwa na Geneva ya Afrika. Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa madiwani hao ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, alisema kumsifu mteule wa Rais ni kuisifu serikali nzima ya Rais Magufuli na haoni sababu ya madiwani wengine kutaka kuchukuliwa hatua.

Aliutaka uongozi wa Chadema Arusha kuacha kufanya siasa za maji taka kwani siasa hizo zimepitwa na wakati na kumsifu mpinzani sio kosa, kwani kuna baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema wamekuwa wakiwasifu mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne na Tano hadharani, lakini hawachukuliani hatua.

No comments:

Post a Comment