Mgogoro huo ambao umedumu takriban mwaka mmoja sasa na ulianzia pale
Profesa Lipumba alipojiuzulu wadhifa wa uenyekiti kabla ya uchaguzi wa
Oktoba 25, 2015 na kusema ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida.
Wakati Profesa huyo alipojiuzulu nafasi hiyo chama hicho kilikuwa katika
wakati mgumu kutokana kukabiliwa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 ambapo CUF
ndicho chama kinachotoa ushindani mkubwa wa kisiasa kwa CCM hasa kwa
upande wa visiwani Zanzibar.
Licha ya CUF kuwa na wakati huo mgumu lakini chama hicho kilipambana na
kuingia katika uchaguzi huo bila ya kuwa na Mwenyekiti lakini hatimaye
kiliweka historia kwa kupata majimbo 10 ya uchaguzi Tanzania Bara na
majimbo 25 kwa upande wa Zanzibar ingawa uchaguzi huo Zanzibar ulifutwa
kwa madai mbalimbali yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Salim
Jecha.
Baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo Zanzibar, ZEC ilitisha uchaguzi
mwingine wa marudio Machi 20 mwaka 2016 lakini chama cha Wananchi CUF
kilisusia uchaguzi huo na hatimaye CCM ikaibuka na ushindi wa kishindo.
Tangu wakati huo CUF bado haiko sawa kutokana na kukukabiliwa na mgogoro
ndani ya chama hicho na wanachama wake kugawanyika katika makundi
mawili, lile linalomuunga mkono Profesa Lipumba ambaye baada ya
kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti alitengua nafsi hiyo na hivi sasa
anatambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ni Mwenyekiti halali wa
chama hicho.
Kundi la pili ni lile linaloungwa mkono na Katibu Mkuu wa CUF Maalim
Seif Sharif Hamad, ambaye anamvuto mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar
na yeye hatambui wadhifa wa Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Profesa Lipumba naye alitangaza kumwajibisha
Maalim Seif Sharif Hamad kwa kumvua wadhifa wake wa Katibu Mkuu kwa
madai kuwa ameshindwa kazi ndani ya chama hicho kwani ameshindwa
kuhudhuria vikao katika ofisi kuu za chama hicho zilizopo Buguruni
Jijijini Dar es Salaam.
Kutokana na hatua hiyo Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Profesa Lipumba
hana mamlaka hayo kwanza siyo mwanachama tena wa CUF, hivyo yeye ndie
Katibu Mkuu wa chama hicho na maamuzi yake ni batili hayakubaliki
kisheria na kikatiba.
Mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa katika ziara yake ya kichama Kisiwa
cha Tumbatu Maalim Seif, alisema mgogoro unaoendelea ndani ya chama
hicho umesababishwa na Msajili wa vyama, Jaji Francis Mutungi kwa
kitendo cha kumhalalisha Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF wakati
alijiuzulu mwenyewe nafasi hiyo lakini pia alishafukuzwa uwanachama na
Baraza Kuu.
Maalim Seif alimshauri Rais wa Jamuhuri ya Muungano Dk. John Pombe
Magufuli kumchukulia hatua Mrajisi wa Vyama vya Siasa Jaji Mutungi
kutokana na kile walichodai kuwa msajili huyo amekuwa akivunja sheria.
“ Tumameshangazwa na kitendo cha rais wa Dk. John Pombe Magufuli
kuwawajibisha watendaji wasio waadilifu huku akimuacha msajili wa vyama
vya siasa,”alisema.
Maalim Seif alisema kuwa msajili huyo ni wakutumbuliwa kama
wanavyotumbuliwa watendaji wengine kwa sababu siyo mwadilifu na
amesababisha mtafaruku mkubwa kwa wananchi na wanachama wa CUF.
“Rais Magufuli anatumbua watendaji ambao siyo waadilifu lakini Msajili
wa Vyama vya Siasa amemuacha kwasababu huyu mtu ametuvuruga na
anaendelea kutuvuruga,” alisema
Alisema msajili huyo amempa uhalali Profesa Ibrahim Lipumba kuwa
Mwenyekiti wa CUF wakati alijiuzulu mwenyewe kabla ya uchaguzi mkuu na
hivi sasa amekuwa akikihujumu chama.
Alisema Lipumba wa sasa ni tofauti na yule wa 2010 kwani hivi sasa
amekuwa akiihujumu CUF kwa makusudi kwa kushirikiana na wadau wake
mbalimbali.
Aidha, alisema baadhi ya askari wa vyombo vya dola wamekuwa wakitumika
kisiasa na wanafanya kazi kwa ubaguzi na kuegemea upande mmoja wa chama
tawala.
Hata hivyo, aliwatoa hofu wafuasi wa chama hicho kuwa yeye ndiye Katibu
Mkuu wa CUF wala wasibabaishwe na kitendo cha Profesa Lipumba kutangaza
kumvua wadhifa huo.
“Eti Lipumba anasema kuwa mimi nimeshindwa kazi akidai kuwa siendi ofisi
kuu ya CUF Buguruni mbona na yeye haji makao makuu ya CUF
Mtendeni……Lipumba hana mamlaka hayo ya kuniondoa nafasi yangu ya ukatibu
mkuu”alisema.
Alihoji kuwa tangu Agosti mwaka 2015 Lipumba hajakanyaga makao makuu ya
CUF Mtendeni yaliyopo Unguja na yeye pia ameshindwa kazi.
Alisema hata kama Lipumba angekuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho
alipaswa kumuita na kumhoji yeye Katibu Mkuu kwa nini haendi ofisi kuu
za chama hicho Buguruni kuliko kuchukua madaraka ya kujaribu kumuondoa
kwenye wadhifa wake.
Akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho kidogo cha Tumbatu Maalim Seif
alielezea kuchukizwa na kitendo cha siasa za chuki na uhasama
zilizotawala kisiwani humo kati ya CCM na CUF na kufikia hatua ya
kupigana na kuhujumiana kwa kuchomeana nyumba moto kwa itikadi za
kisiasa.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, wananchi wa kisiwa
kidogo cha Tumbatu wamegawanyika kisiasa kati ya Wananchi wa Tumbatu
Uvuvini ambako ni ngome ya CCM na Tumbantu Jongowe ambayo ni ngome ya
CUF.
No comments:
Post a Comment