Wednesday, April 5, 2017
ARUSHA KUKUSANYA BILIONI MOJA YA KODI YA MAJENGO
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo amewaagiza watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kushirikiana na watumishi wa Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa kukusanya Tsh Bilioni moja za kodi ya majengo kwa kipindi cha Mwezi wa Nne.
Rc Gambo ameyasema hayo wakati wa kikao kazi na watendaji wa Kata, Mitaa, Wahasibu wa Mapato, wataalamu wa Mipango Miji pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha kilichofanyika mapema wiki hii.
Akizungumza katika Kikao hicho cha kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto ya kutokusanyika kwa Kodi ya Majengo kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 Rc Gambo amesema hata kama hata kama chanzo hicho kimehamishiwa TRA, Halmashauri ya Jiji bado ina mchango mkubwa katika kufikia Malengo yaliyowekwa kwa kushirikiana na wataalamu wa TRA kwenye Kata na Mitaa yote ya Jiji.
Aliongeza kuwa Jiji kuna watumishi wengi ambao wanafahamu kila nyumba katika mitaa yote ya Jiji na wamekuwa wakifanya kazi hii kwa kipindi kirefu hivyo wana uzoefu wa kutosha na ushiriki wao katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka wa Fedha ni muhimu sana ili kwa pamoja tuweze kufanikiwa kukusanya maduhuli ya Serikali kwa ufanisi.
Alisema maeneo yote ambayo hayajapimwa kila mmiliki wa jingo atalipia Tsh 15,000 na maeneo ambayo hayajapimwa ila yamefanyiwa Uthamini watalipa kwa kiwango walichokadiriwa na kwa maeneo yaliyopimwa ya kwa viwango vya juu tunaangalia utaratibu mzuri wa kukusanya hivyo kila mmiliki wa jingo atomize wajibu wake kwa kulipa kodi hii.
“Hapa tunachohitaji ni kuunganisha nguvu ya pamoja ili tuweze kufikia Malengo na sio kwa sababu Chanzo hiki kiko chini ya TRA kwa sasa basi Jiji basi Taasisi zingine zisitoe Ushirikiano mimi kama Msimamizi wa shughuli za Serikali ntashirikisha kila Taasisi inayohusika ili kufanikisha Malengo ya ukusanyaji na sio katika chanzo hiki tu bali katika Vyanzo vyote alisema Gambo”.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba kazi hiyo itafanyika kwa kadiri ya Maelekezo waliyoyapokea na kwamba ana imani kubwa na wataalamu wa Jiji kwa kuwa wamekwishashiriki mazoezi kazi mbalimbali na kuleta mafanikio makubwa katika Wilaya hii.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha bwana. Athumani J. Kihamia aliongeza kuwa atawasimamia watendaji ipasavyo katika kukusanya kodi ya Majengo na ataendelea kuwajengea uwezo ili kuongeza ufanisi katika zoezi hilo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Arusha, bwana Apili Mbarouk ameelezea hali ya ukusanyaji wa chanzo hiki kwamba hairidhishi kwani mpaka sasa wamefanikiwa kukusanya Tsh Mil 200 tu wakati malengo ya Ukusanyaji wa mwaka wa Fedha unaoishia Juni 2017 ni Tsh Bil 5 hivyo ni vyema kuongeza nguvu ili kufikia Malengo.
Kikao kazi hiki ni muendelezo wa wa Vikao vinavyoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Gambo katika kutatua kwa pamoja changamoto za sekta mbalimbali katika Mkoa huu ili kuleta Mafaniko ya pamoja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment