Friday, March 3, 2017

WABUNGE ,MEYA WAPINGA TANROADS KUPEWA MAJENGO



WABUNGE mkoani Rukwa na Meya wa Manispaa ya Sumbawanga wamepinga uamuzi wa serikali kuwapa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Rukwa majengo ya kambi yaliyokuwa yakitumiwa na wajenzi kutoka China.

Viongozi hao wamesema, watapambana ili majengo hayo yatumike kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Sumbawanga.

Majengo ya kambi hiyo yapo nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga na Kampuni ya Ujenzi ya China ya Jiangxi Geo –Engineering (Group) Corporation ambayo inajenga barabara kutoka Mji wa Sumbawanga ikipitia kijiji cha Chala hadi kijiji cha Kanazi wilayani Nkasi yenye urefu wa kilomita 75 kwa gharama ya Sh 78,840,586,371.

Wanasiasa hao walicharuka katika kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya mkoa wa Rukwa kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 kilichokutana juzi mjini hapa baada ya Meneja wa Tanroads mkoa wa Rukwa, Masaku Mkina kuwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa tayari serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano imekubali majengo hayo yatumike kama ofisi za Tanroads mkoa wa Rukwa pamoja na maabara ya udongo ya kanda.

Mkina alikuwa akijibu swali la Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda aliyetaka kufahamu Tanroads ina mikakati gani baada ya wajenzi wa Kichina wanaojenga miradi ya barabara kwa kiwango cha lami watakapomaliza kazi yao ili majengo ya kambi yatumike na halmashauri zilizopo mkoani humo kwa shughuli za maendeleo.

Akijibu alizitaka halmashauri za wilaya hiyo zinazohitaji majengo hayo kuwasilisha maombi yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano kwa kuwa waombaji ni wengi.

“Sisi Tanroads tumeshatuma maombi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano na ametukubalia ombi letu kuwa majengo ya kambi hiyo tuyatumie kama ofisi ya Tanroads mkoa wa Rukwa,” amesisitiza.

Kauli hiyo ilimuinua Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Malisawa ambaye aling’aka na kusema kuwa hakubaliani na uamuzi huo huku akisisitiza kuwa uvumilivu umemshinda .

“Mwaka 2007 Serikali ilitoa miongozo kuwa haitatoa fedha za mfuko wa barabara kwa wilaya isiyokuwa na Hospitali ya Wilaya, Manispaa ya Sumbawanga haina hospitali ya wilaya hivyo tukalazimika kuingia mkataba na Hospitali Teule ya Dk Atman (inamilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga ) mkataba ambao hauna tija kwetu,” ameeleza.

Ameongeza kuwa mchakato wa kuhakikisha majengo ya kambi yatumike kama Hospitali ya Wilaya ulishaanza tangu wakati wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay. Akichangia Mbunge wa Sumbawanga, Aeish Hilaly (CCM) alisema kuwa eneo ilipo kambi hiyo ni mali ya Halmashauri ya Sumbawanga ambayo ililipia fidia.

Licha ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven kuwaomba wajumbe wa bodi hiyo ya barabara kulijadili hilo siku inayofuata katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Rukwa (RCC) lakini Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Tixon Nzunda alisimama na kutaka Meneja Tanroads mkoa wa Rukwa (Mkina ) asishambuliwe.

“Tusimshambulie Meneja wa Tanroads (Mhandisi Mkina) kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na RAS wamelifanyia kazi suala hilo kwa kipindi kirefu. Mimi binafisi niliwasiliana na Katibu Mkuu (Wizara ya Ujenzi ) mara sita kisha nilimwandikia barua tatu ambazo hazikujibiwa nikalazimika kufunga safari ya kwenda kumuona mwenyewe… nilipozungumza naye aliniambia nimekusikia ngoja niwasiliane na mamlaka za juu,” ameeleza.

Aliongeza kuwa baada ya hapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilipata barua kutoka Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano ikieleza kuwa uwezekano ni mdogo wa kupata majengo ya kambi hiyo kwa kuwa maandalizi yote yamekamilika ya kukabidhi majengo hayo ofisi za Tanroads za mkoa na maabara ya udongo ya kanda.

No comments:

Post a Comment