WAZIRI WILIAM LUKUVI.
SERIKALI imetishia kutengua umiliki na kupiga mnada viwanja vya makazi na biashara zaidi ya 50 katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai, huku ikiwaweka njia panda wananchi 42 ambao wameacha magofu ya nyumba zao.
Katika orodha ya viwanja vinavyotajwa kipo kinachodaiwa kumilikiwa na Wakili Jenerali Ulimwengu ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya hiyo.
Uamuzi wa kutaka kutengua umiliki wa viwanja hivyo na kuviuza kwa watu wenye uwezo wa kuviendeleza ulitangazwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa, wakati wa kikao cha muendelezo wa kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi.
“Kuna watu 50 ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu na wengine 42 wameendeleza, lakini hawajamalizia na wametelekeza. Orodha hii si kwa nia mbaya ila ni kuwashtua huko walipo wajitokeze waje kuviendeleza au kama hawapo tuwape watu wengine,” alisema.
"Nimekuwa nikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Hai mjini na nje ya mji mdogo wa Bomang’ombe, baadhi yao wakiwa wakweli na wengine siyo wa kweli wanaodai kuuziwa viwanja bila utaratibu maalumu wa jambo linalopelekea makazi yao kushindwa kuendelezwa kama inavyo hitajika."
“Niwe muwazi kuwa kuna baadhi ya viwanja vilivyouzwa mara mbili na kuleta usumbufu unao weza kuibua migogoro na chuki na ukiangalia hilo ni ofisi ya ardhi ndiyo waliofanya mchezo huo, hivyo nawataka kutatua na kugawa maeneo hayo kwa utaratibu unao kubalika.”
"Kwa wake waliokwisha nununua maeneo au kupewa maeneo na kushindwa kuyaendeleza yatachukuliwa na kupewa watu wenye uwezo wa kuyaendeleza ili kuruhusu mji kukua kwa mpangilio unao hitajika," alisema.
Awali, Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Hai, Poesent Majumba, alikiri kuwapo wananchi wanaolalamika maeneo yao kuchukuliwa au kuuzwa pasipo kujua, hivyo kuahidi kutatua matatizo hayo ili haki zao ziweze kupatikana kwa wakati.
No comments:
Post a Comment