Friday, March 17, 2017

VIGOGO PRESHA JUU YA PANGA LA CCM ZANZIBAR


Hamkeni si shwari tena! Hivyo ndivyo inavyoelezwa kuhusiana na hali ya hofu inayodaiwa kuwakumba baadhi ya makada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar.

Hali hiyo inatokana na kuundwa kwa kamati maalumu ya kufuatilia mwenendo wa kimaadili wa baadhi ya makada wanaotuhumiwa kukiathiri chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Jumamosi iliyopita, CCM kupitia kamati yake ya maadili na usalama iliwachukulia hatua kali baadhi ya wanachama wake waliohusishwa na makosa mbalimbali ya kimaadili, ikiwamo wengine kufukuzwa uanachama.

Wanachama waliofukuzwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.

Wengine ni wenyeviti wa mikoa wa chama hicho, Jesca Msambatavangu (Iringa), Christopher Sanya (Mara) na Erasto Kwilasa wa Shinyanga.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema CCM imeunda pia kamati ndogo itakayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, kuangalia hali ya kisiasa na kufanya tathmini ya uchaguzi Zanzibar.

Kamati hiyo ambayo pia itawabaini wanachama waliokiuka maadili, inaundwa pia na aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amiri Kificho, Daud Ismail, Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Maua Abeid Daftari, Stephen Wasira na Zakia Meghji.

Katika uchunguzi wake uliohusisha mahojiano na baadhi ya makada wa chama hicho visiwani Zanzibar, Nipashe imebaini kuwa kuundwa kwa kamati ya Mangula na rejea ya kile kilichowakuta kina Simba na Madabida, kumezua hofu kubwa kwa baadhi ya makada wao wanaoonyoshewa vidole kwa tuhuma za ukiukaji wa maadili ya chama na usaliti wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Imeelezwa kuwa baadhi ya wale walio na hofu ni pamoja na wale wanaotuhumiwa kuwa na uswahiba na viongozi wa mahasimu wao wakuu, Chama cha Wananchi (CUF), akiwamo Maalim Seif Shariff Hamad aliyekuwa akichuana na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

“Kama ilivyokuwa Bara, huku (Zanzibar) wapo pia waliokuwa wameng’ang’ania kubaki kwenye kambi za watia nia waliokatwa majina yao wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM hata baada ya Magufuli kupitishwa.

Hawa pia wamejawa hofu kwa sasa,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.

Aidha, chanzo kingine kilibainisha kuwa miongoni mwa makada waliojawa hofu ya kukutwa na ‘panga’ baada ya uchunguzi wa kamati ya Mangula ni pamoja na wale ambao kauli na matendo yao yaliashiria kutomuunga mkono Dk. Shein.

“Wapo pia walioiweka CCM katika wakati mgumu kipindi cha uchaguzi ule uliofutwa wa Oktoba 25, 2015 kwa sababu nyendo zao ziliashiria kumuunga mkono Maalim Seif.

Hawa pia wamejawa hofu kuhusiana na hatima yao ndani ya CCM,” kilieleza chanzo hicho.

Dk. Shein na Maalim Seif walichuana vikali katika uchaguzi mkuu wa awali uliofanyika Oktoba 25, kabla ya kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutokana na kile alichoeleza kuwapo kwa kasoro nyingi.

Hata hivyo, CUF ilipinga madai ya Jecha na kumtuhumu kuvuruga uchaguzi huo ili kuiokoa CCM iliyokuwa ikidaiwa kuzama kutokana na Maalim Seif kuelekea kushinda.

Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka jana, CUF ilisusia kwa madai kwamba haukuwa halali hivyo ZEC kumtangaza Dk. Shein kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 91 ya kura halali zilizopigwa.

NAIBU KATIBU MKUU ANENA
Akizungumzia kuundwa kwa kamati ya Mangula na hofu ya kutimuliwa baadhi ya wanachama, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai, alisema hakuna sababu kwa mwanachama yeyote mtiifu kuwa na hofu na kwamba anapongeza kilichofanyika kwa sababu ni uamuzi wa busara wenye lengo la kuimarisha chama.

Vuai alisema hatua za kuimarisha chama chao Bara zimeshachukuliwa, hivyo ni busara kwa jambo hilo kufanyika pia visiwani Zanzibar.

“CCM yote ni moja, kilichofanyika Bara kwa lengo la kujenga na kukiimarisha chama ni vyema na Zanzibar kikafanyika pia,” alisema.

Aidha, aliwashauri wanachama wenzake kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo ndogo ya Mangula ili ifanikishe malengo yake.

Katibu wa Oganaizesheni na Idara Maalum ya CCM Zanzibar, Haji Mkema Haji, alisema kamati ya Mangula inapaswa kupewa ushirikiano wa kutosha kwa sababu ni muhimu kwa mustakabali wa chama.

Alisema kamati hiyo ikifanikisha vyema kazi yake, maana yake mambo yote yenye upungufu yatabainika na hatua kuchukuliwa kwa nia ya kuiimarisha CCM.

Kada mwingine wa CCM, Mohammed Said Mohammed, alisema tayari wasaliti wa chama kwa upande wa Bara wamechukuliwa hatua, hivyo ni wakati muafaka kwa hatua kama hizo kuchukuliwa Zanzibar ambako pia kuna wanachama wanaokirudisha nyuma chama kutokana na usaliti wanaoufanya.

Mohammed ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, alisema badala ya wahusika wa vitendo vya usaliti kutapatapa kwa hofu, jambo la muhimu kwao ni kujiandaa kwa lolote kwa sababu ni lazima kamati hiyo itawabaini kupitia uchunguzi wake.

No comments:

Post a Comment