Utangulizi
Wiki na miezi iliyopita kumekuwepo na mijadala mizito ya kisiasa na
kitaifa juu ya masuala ya upungufu wa chakula Tanzania.
Taaarifa za
upungufu wa chakula mwanzoni zilikataliwa na viongozi wa juu wa serikali
lakini baadae walikiri kuwepo kwa upungufu wa chakula nchini. Mwishoni
mwa mwezi Januari 2017, Waziri wa Chakula, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles
Tizeba aliliambia bunge kwamba utafiti uliofanywa na Wizara kwa
kushirikiana na wadau kadhaa 1 , umegundua kwamba Wilaya 55 (kati 169 za
Tanzania Bara na Visiwani) zilikumbwa na njaa, na tani “35,491 za
nafaka zinahitajika kusambazwa kati ya mwezi wa pili na wa nne mwaka
2017 ili kukabiliana na upungufu huo uliowakumba watu 1,186,028” 2
katika Wilaya hizo.
Waziri Tizeba alilalamikia kupanda kwa bei za vyakula katika maeneo
mengi na alisema hii inasababishwa na wafanyabiashara wasio waaminifu
wanaotumia mianya ya njaa, pamoja na uhitaji mkubwa wa mahindi katika
nchi jirani. Matokeo yake ni kusababisha bei za ndani kupanda. Aliongeza
kwamba “Serikali imeanza kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo ambayo ni
pamoja na kutoa chakula kutoka hifadhi za taifa na kuuza kwa bei nafuu
katika maeneo yaliyo athirika.”
Sintofahamu hii juu ya hali ya chakula nchini imetokea katika kipindi
ambacho uchumi wa Tanzania umekua kwa kasi nzuri ya asilima saba kwa
mwaka. Lakini ukuaji huu haujafanikiwa kuondoa umasikini kwa kiwango
kilichotarajiwa na wengi. Asilimia 68 ya wananchi bado wanaishi chini ya
kiwango cha umasikini cha $1.25 kwa siku 3 . Pamoja na hayo kiwango cha
udumavu kimeendelea kuonekana kwa watoto chini ya miaka 5 4 ,
ukiachilia mbali mafanikio madogo yaliyopatikana katika miaka ya
karibuni kwenye utoaji wa lishe nchini. Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya
Tanzania (NBS) na UNICEF wanakadiria kuwa robo tatu ya watoto wote wa
Tanzania asilimia 74) wanaishi kwenye umasikini mkubwa 5 .
Muhtasari huu unawasilisha takwimu za maoni ya wananchi na uzoefu wao
katika hali ya upungufu wa chakula na sababu zake. Ni kaya ngapi na
jamii zipi ambazo zimekumbwa na njaa? Ni vyakula vipi vilivyo adimu
kupatikana? Na ni kwa namna gani bei za vyakula zimepanda ikilinganishwa
na miezi michache iliyopita?
Takwimu za muhtasari huu zimetokana na utafiti wa Twaweza wa Sauti za
Wananchi. Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi mkubwa unaotumia
simu za mkononi. Uwakilishi huu ni wa Tanzania bara. Maelezo zaidi juu
ya utafiti huu yanapatikana katika tovuti ya www.twaweza.or.tz/sauti. Takwimu za muhtasari huu zilikusanywa katika awamu ya pili ya kundi la pili la Sauti za Wananchi.
- Wahojiwa 1,800, awamu ya 13 ya kupigiwa simu kwa kundi hili la wahojiwa, kati ya tarehe 14 - 26 Septemba 2016.
- Wahojiwa 1,610, awamu ya 16 ya kupigiwa simu kwa kundi hili la wahojiwa, kati ya tarehe 9 - 15 Februari 2017.
Matokeo makuu ni:
- Kaya nane kati ya kumi (asilimia 80) zimeripoti kwamba kipato chao hakikidhi mahitaji yao ya kila siku.
- Kaya nane kati ya kumi (asilimia 79) huweka akiba ya chakula kwa ajili ya kijitosheleza ifikapo vipindi vya njaa.
- Wahojiwa wengi wa Sauti za Wananchi (asilimia 78) wanaripoti upungufu wa chakula katika maeneno wanayoishi
- Bei ya mahindi imepanda mara mbili katika kipindi cha miaka miwili na kusababisha ongezeko la bei katika bidhaa.
- Kaya saba kati ya kumi (asilimia 69) zilihofia kukumbwa na njaa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
- Hali ya upungufu wa chakula imekua mbaya zaidi katika kipindi cha mwezi wa Septemba mwaka 2016 hadi Februari, 2017.
Mambo nane muhimu kuhusu hali ya chakula Tanzania
Jambo la 1: Kaya nane kati ya kumi zimeripoti kwamba kipato chao hakikidhi mahitaji yao ya kila siku.
Mwezi Septemba mwaka 2016 kaya nane kati ya kumi (asilimia 80)
ziliripoti kuwa na kipato kisichokidhi mahitaji yao ya kila siku.
Takwimu hizi zinatofautiana kidogo katika kaya za mijini na zile za
vijijini au kati ya kaya masikini na kaya tajiri.
Kielelezo cha 1: Je kipato kinachopatikana katika kaya kinatosha kukidhi mahitaji ya kila siku ya nyumbani?
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016)
Kaya tano kati ya sita (asilimia 85) zinasema kwamba kipato kinapopungua
wanalazimika kubana matumizi. Idadi ndogo inasema watakopa bidhaa
(asilimia 6) na wengine huripoti kwamba watakopa fedha zaidi (asilimia
2).
Walipoulizwa kukadiria ni kiasi gani cha fedha kingetosha kwa ajili ya
mahitaji ya kaya ya kila siku, wastani wa makadirio yote yalikua
shilingi 1,777 kwa mwanakaya au shilingi 10,662 kwa kila kaya 6 . Kwa
mwanakaya anaeishi mjini makadirio yalikuwa juu kidogo (shilingi 2,247)
kuliko kijijini (shilingi 1,579). Makadirio pia yalikuwa makubwa zaidi
kutoka kwenye kaya zenye uwezo (asilimia 20 ya waliokuwa na utajiri wa
juu sana - Shilingi 2,304) ukilinganisha na kaya masikini (asilimia 20
ya waliokuwa na umasikini wa chini kabisa - Shilingi 1,577).
Jambo la 2: Wananchi tisa kati ya kumi wanaona ni jukumu lao wenyewe kuhakikisha wana fedha za kutosha za kukidhi mahitaji ya kaya zao
Idadi kubwa ya wananchi (asilimia 87) wanasema iwapo watakosa fedha za
kukidhi mahitaji ya chakula kwa ajili ya familia zao, hawatarajii watu
wengine kulichukua jukumu hilo. Hata hivyo, asilimia 17 ya wanawake na
asilimia 9 ya wanaume wangetarajia msaada kutoka nje.
Kielelezo 2: Iwapo ungekuwa huna
pesa za kukidhi mahitaji ya chakula kwa ajili ya familia yako pamoja na
kaya yako, je unadhani ni jukumu la mtu kukusaidia au ni jukumu lako
mwenyewe?
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016)
Miongoni mwa wale wananchi wachache (asilima 13) wanaofikiri kwamba ni
jukumu la mtu mwingine kuwasaidia katika hali hiyo, nusu yao (asilimia
49) wamesema ni wajibu wa serikali kutoa msaada. Idadi ndogo wamesema ni
wajibu wa wanandugu (asilimia 36) au marafiki na majirani (asilimia 7).
Jambo la 3: Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kaya moja kati ya nne imepokea fao, faida au pesa kutoka kwenye miradi ya serikali
Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kuanzia mwezi wa tisa 2015 mpaka
mwezi wa tisa 2016, asilimia 25 ya kaya zimepokea fao, faida au pesa
kutoka katika vyanzo vifuatavyo:
- Sare za shule, kadi ya matibabu, chakula na kadhalika kutoka kwenye Mpango wa Watoto Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu
- Nafaka za bure kutoka kwa viongozi wa kijiji na Wakala Wa Taifa Wa Hifadhi Ya Chakula (NFRA)
- Chakula cha shule kinachotolewa na Mpango wa Chakula Shuleni
- Kazi za jamii zinazotolewa na Tanzania Social Action Fund (TASAF)
- Pesa zinazotolewa na TASAF kwa ajili ya kunusuru kaya masikini
- Vocha za mbolea/mbegu zinazotolewa na Mpango wa Taifa wa Ruzuku na Kilimo
- Malipo ya mafao kutoka Mfuko wa Pensheni wa Taifa (NSSF)
- Malipo ya mafao kutoka Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF)
Kielelezo 3: Mafao au faida zilizopokelewa ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita
(Asilimia ya kaya zinazopokea mafao haya)
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 13 (Septemba 2016)
Jambo la 4: Kaya nane kati ya kumi huweka akiba ya chakula
Kaya nane kati ya kumi (asilimia 79) zimeripoti kwamba wana hifadhi
chakula kwa ajili ya dharura au kuepukana na njaa. Wananchi wengi zaidi
wa vijijini huhifadhi (asilimia 87) kuliko wa mijini (asilimia 61) na
kaya masikini huhifadhi kuliko kaya tajiri. Uhifadhi wa chakula pia uko
juu kwa kaya ambazo hutegemea zaidi kilimo kama sehemu kubwa ya kipato
chao (asilimia 92) kuliko kaya ambazo hutegemea vyanzo vingine vya
mapato kama vile biashara au ajira (asilimia 49).
Kielelezo cha 4: Je, kaya yako huhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi wakati wa dharura au njaa?
(Asilimia iliyojibu ndiyo)
Chanzo cha takwimu: Utafiti wa Sauti za Wananchi - Awamu ya 16 (Februari 2017)
No comments:
Post a Comment