Tuesday, March 21, 2017

SERIKALI YAKANA KUMSHIKILIA YUSUPH MANJI

Sakata la kushikiliwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Yusufu Manji limeendelea kuchukua sura mpya, safari hii yakiibuka mabishano Mahakama Kuu baada ya Serikali kukana kumshikilia.

Mabishano hayo yameibuka jana kati ya mawakili wa Serikali na mawakili wa Manji baada ya mfanyabiashara huyo kufungua maombi juma lililopita akihoji uhalali wa kushikiliwa na Uhamiaji.

Manji aliyefungua maombi hayo mahakamani hapo kupitia Wakili wake Hudson Ndusyepo, anaiomba mahakama iiagize Uhamiaji afikishwe mahakamani ili mahakama iamue uhalali wa kushikiliwa kwake na kisha iamuru aachiwe huru.

Kutokana na maombi hayo, Jaji Ama-Isario Munisi, aliwaamuru wajibu maombi kuwasilisha hati zao za kiapo kinzani dhidi ya maombi hayo na kupanga kuyasikiliza jana mchana.

Wajibu maombi ni Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.

Hata hivyo jana Serikali katika majibu yake kupitia  hati ya kiapo kinzani cha Ofisa Uhamiaji, Anorld Munuo, ilikana kumshikilia mfanyabiashara huyo. Mbali na kiapo hicho, Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekoma, alisisitiza kuwa mfanyabiashara huyo hashikiliwi na yuko huru.

Maelezo hayo ya Serikali yalipingwa vikali na mawakili wa Manji, Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo, ambao kwa nyakati tofauti walisisitiza kuwa hadi jana mfanyabiashara huyo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, kwa matibabu, akiwa chini ya ulinzi wa maafisa Uhamiaji.

No comments:

Post a Comment