WINGA machachari na tegemeo wa Yanga, Simon Msuva, amesema ana maisha
mafupi ya kuendelea kuwepo katika timu hiyo huku akiendelea kuweka
mipango yake ya kuondoka Jangwani. Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya
mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumalizika kati ya Yanga na Zanaco ya
Zambia iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na
matokeo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Nyota huyo, hadi hivi sasa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea
kuichezea timu hiyo inayofundishwa na Mzambia, George Lwandamina.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema ana malengo na ndoto
nyingi za kucheza soka la kulipwa, hivyo hategemei kukaa muda mrefu
Yanga.
Msuva alisema ni mapema kuweka wazi katika kipindi hiki ambacho bado ana
mkataba na Yanga, kila kitu atakiweka wazi mara baada ya mkataba wake
kumalizika. Aliongeza kuwa, ana ofa nyingi amezipata ndani na nje ya
nchi ambazo kwa sasa amezifanya siri huku akiendelea na majukumu mengine
ya kuipambania timu yake.
“Hivi unavyotegemea mimi nitaichezea Yanga milele? Hapana, nina mipango
mingi niliyoweka mara baada ya mkataba wangu wa mwaka mmoja kumalizika.
“Nisingependa kuweka wazi kila kitu changu ninachokifanya katika kipindi
hiki, zipo ofa nyingi lakini huu siyo muda wake, kwani nimebakisha
mwaka mmoja wa kuendelea kuichezea Yanga.
“Bado ninaendelea kuipenda timu yangu ya Yanga inayoniajiri na kunilipa
mshahara mzuri, lakini ijulikane kuwa mimi sitaichezea Yanga milele,”
alisema Msuva.
No comments:
Post a Comment